6/recent/ticker-posts

ACT Wazalendo yaendelea na Mazungumzo ya Mwafaka wa Kisiasa Zanzibar



Yataja Katiba na Uchaguzi Kuwa Chanzo cha Migogoro

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa na aliyekuwa Mgombea Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Othman Masoud Othman, amesema kuwa mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, chama chake kilishiriki katika mazungumzo ya kisiasa yenye lengo la kutafuta mwafaka wa kudumu wa kisiasa Zanzibar.
Othman amesema kuwa mazungumzo hayo yamefikia hatua muhimu na ndani ya muda mfupi ujao, wananchi watajulishwa rasmi kuhusu yaliyofikiwa baada ya pande zote mbili za kisiasa kukamilisha taratibu zao za ndani.
Akizungumza leo tarehe 11 Februari 2026 alipokuwa akikutana na viongozi wa chama wa wilaya ya Chake Chake na Mkoa wa Kusini Pemba katika ukumbi wa ofisi ya Jimbo la Chambani, Othman alisema kuwa mazungumzo hayo yaliongozwa naye pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Juma Duni Haji, huku upande wa CCM ukiongozwa na Marais Wastaafu Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein.
Kushuka kwa Imani ya Wananchi Kwenye Uchaguzi
Akitaja hoja kuu zilizojadiliwa, Othman alisema pande zote mbili zilikubaliana kuwa kuna kushuka kwa kiwango cha imani ya wananchi katika chaguzi za Zanzibar, hali ambayo imeendelea kujirudia kila baada ya miaka mitano.
Alisema kuwa mazungumzo hayo yalilenga kutafuta suluhisho la pamoja la kurejesha imani hiyo kwa wananchi, akisisitiza kuwa demokrasia haiwezi kusimama bila wananchi kuwa na imani na mchakato wa uchaguzi.
*Katiba ya Zanzibar Yatajwa Kupitwa na Wakati*
Katika hatua nyingine, Othman alisema kuwa walijadili kwa kina mapungufu ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, akieleza kuwa katiba hiyo imepitwa na wakati na haikidhi mahitaji ya kisiasa na kijamii ya Zanzibar ya sasa.
Alisema katiba hiyo imempa Rais mamlaka makubwa kupita kiasi, hali inayomfanya kuwa kama mfalme asiyeweza kuwajibishwa, jambo ambalo pande zote mbili katika mazungumzo walilikiri kuwa ni tatizo linalohitaji marekebisho ya msingi.
Mfumo wa Uchaguzi Walaumiwa
Othman aliongeza kuwa walijadili pia mfumo mzima wa uchaguzi Zanzibar, akieleza kuwa licha ya kufanyiwa marekebisho mara kadhaa, bado mfumo huo haujatoa nafuu yoyote kwa wananchi wala vyama vya siasa.
Alisema migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza kila uchaguzi inatokana na mfumo mbovu wa uendeshaji wa chaguzi na sheria kandamizi, hasa kwa vyama vya upinzani.

Hofu ya Utekelezaji wa Makubaliano
Sambamba na hayo, Othman alisema kuwa katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zilieleza hofu na wasiwasi juu ya utekelezaji wa makubaliano, hali iliyowafanya wakubaliane kuweka ratiba maalumu ya utekelezaji huku kila upande ukipewa jukumu la kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa ipasavyo.
*Kuhusu suala la kuingia au kutokuingia serikalini*
Othman alisema kuwa ACT Wazalendo wanasubiri kuona hatua za vitendo za utekelezaji na pindi zitakapokamilika wananchi wataelezwa msimamo wa mwisho wa chama.
Amesema ni lazima uchaguzi wowote mkuu ujao Zanzibar uendeshwe kwa makubaliano mapya yaliyoandikwa na kukubalika na pande zote.
Mahakama na Haki ya Zanzibar
Katika hotuba yake, Othman alieleza kwa masikitiko namna Zanzibar inavyoendelea kuporwa haki yake, akitaja kushindwa kwa Mahakama Kuu ya Zanzibar kusikiliza baadhi ya mashauri muhimu yanayohusu masuala ya Muungano.
Alitoa mfano wa kesi za wagombea wa ubunge zilizotupiliwa mbali, akisisitiza kuwa athari zake haziiathiri ACT Wazalendo pekee bali ni mwendelezo wa kuinyima Zanzibar haki yake ya kikatiba.
Alisisitiza kuwa chama chake kitaendelea kukosoa hadharani na kupigania haki za Zanzibar bila woga wala kuchoka.
Wito kwa Mahakama Kujitathmini
Aidha, Othman aliitaka Mahakama kujitathmini na kuacha kutumika kisiasa, akisema kufanya hivyo kunavunja hadhi ya chombo hicho ambacho ndicho kimbilio la mwisho la wananchi.
Alieleza kuwa inasikitisha kuona yeye binafsi akiwa wakili aliwahi kushuhudia kesi ikiahirishwa kwa sababu jaji aliomba ruhusa ya kwenda kumpokea mgombea wa urais.
Kwa kumalizia, Othman alitoa wito kwa watendaji wa Mahakama kuendelea kuwa waadilifu, jasiri na wenye msimamo, na kukataa kutumika kisiasa ili kulinda heshima ya chombo hicho na matumaini ya wananchi wa Zanzibar.
Imetolewa na Idara ya Habari na Uenezi.ACT Wazalendo
11 February 2026



 

Post a Comment

0 Comments