NA FAUZIA MUSSA
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi zisizo za Kiserikali (NGOs) na washirika wa maendeleo imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa vya kisasa vya kuchujia maji 'TAB Cap-Type Water Purifier' iliofanyika Taasisi ya Korea Culture Mbweni Mrajisi wa Asasi za Kiraia Zanzibar Ahmed Khalid Abdulla alisema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wote Unguja na Pemba, na kusisitiza kuwa maji ni uhai na msingi wa afya ya jamii.
Alieleza kuwa Serikali imekuwa ikichukua juhudi mbalimbali ikiwemo kuimarisha sera, kuweka mazingira wezeshi, na kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha changamoto ya maji safi inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaamini kuwa bila maji safi na salama, hatuwezi kuzungumzia afya bora, maendeleo ya binadamu wala ustawi wa jamii. Ndiyo maana tunaendelea kufungua milango kwa Taasisi zisizo za Kiserikali na washirika wa maendeleo ili tushirikiane kwa karibu zaidi,” alisema Mrajisi huyo.
Alifafanua kuwa hafla hiyo imekuja wakati muafaka, hasa ikizingatiwa kuwa visiwa vya Zanzibar vinaelekea kwenye kipindi cha mvua, ambacho kwa kawaida huambatana na changamoto za maji machafu, mlipuko wa maradhi yatokanayo na maji na vyakula visivyo salama, pamoja na athari za kiafya kwa watoto, wazee na makundi yenye uhitaji maalum.
"Matumizi sahihi ya kifaa hichi yanaweza kusaidia kupunguza au kudhibiti mlipuko wa maradhi yanayotokana na maji na vyakula visivyo safi, ikiwemo kuhara, kipindupindu, homa ya matumbo na magonjwa mengine."
Pamoja na hayo alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa NGOs ili ziweze kufikia malengo yao kwa ufanisi, hususan katika sekta nyeti kama maji, afya, elimu na ustawi wa jamii.
Alisema uwepo wa Taasisi zisizo za Kiserikali nchini ni fursa kubwa kwa Serikali, kwani zinachangia kwa vitendo katika kusaidia jamii, hasa maeneo yenye changamoto za kimaendeleo.
“Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa NGOs na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kusaidia zaidi katika miradi mbalimbali ya kijamii. Lengo letu ni kuona mchango wao unaleta matokeo chanya kwa wananchi,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Mrajisi aliitaka taasisi ya Korea Culture, kushirikiana na viongozi wa shehia kutambua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo husika, ili kupata njia sahihi za kuwasaidia kulingana na mahitaji halisi ya jamii.
Alisema ni muhimu kwa wadau wa maendeleo kuelewa mazingira ya wananchi kabla ya kuingiza miradi, ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na yenye tija kwa walengwa.
Mrajisi aliwahimiza wananchi waliopokea mashine hizo kuzitumia ipasavyo kwa kufuata miongozo iliyotolewa, akisisitiza kuwa maji yanayochujwa kwa kifaa hicho ni safi na salama kabisa kwa matumizi ya kunywa.
“Hata mimi mwenyewe pamoja na Diwani wa Wadi ya Chukwani tulijaribu kunywa maji yaliyochujwa kwa kifaa hiki, na mpaka sasa tuko salama na tunaendelea na majukumu yetu kama kawaida,” alisema.
Aliongeza kuwa endapo wananchi wataendelea kutumia maji yasiyo safi na salama, Serikali na jamii kwa ujumla italazimika kugharamia matibabu makubwa, jambo ambalo lingeweza kuepukika kwa kuchukua tahadhari mapema.
“Maji yasiyo safi ni gharama kubwa kwa afya ya jamii. Tukitumia maji salama, tunapunguza mzigo wa magonjwa na gharama za matibabu,” aliongeza.
Akizungumzia kuhusu kifaa hicho Mkurugenzi Korea Culture Master Kim Jong Ho alisema ni ubunifu uliolenga kuchuja maji yenge vumbi au vijidudu na kuyafanya kuwa safi kwa matumizi ya binadamu licha ya kuwa njia ya kuchemsha inashauriwa zaidi.
Alieleza kuwa vifaa hivyo vinatolewa bila malipo kwa wakazi wa maeneo yaliyolengwa, ikiwa ni sehemu ya mchango wa tAB, Korea Culture na KOICA katika kuimarisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar.
Alifahamisha kuwa kifaa hicho kinatumika bila umeme kwa kufungwa na kufunguliwa kwa urahisi kwenye dumu kulingana na mahitaji ya mtumiaji.
"Kifaa hichi kina filters tatu ambazo zinapaswa kubadilishwa kila mwezi, Filters hizi zitapatikana hapa hapa corea culture kwa gharama nafuu ili muendelea kukitumia kwa muda mrefu." Alisisitiza Kim
Aidha aliwasisitiza kusafisha vyombo vya kuhifadhia maji mara kwa mara ili kuepuka uchafuzi wa pili.
Kwa upande wake, mvumbuzi wa kifaa hicho kutoka kampuni ya T.A.B Ltd, Oh Hwan Jong aliwaomba wananchi waliopokea mashine hizo kuzitunza na kuzitumia kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa, ikiwemo kubadilisha filter kwa wakati uliopendekezwa.
“Mashine hii ni mfano mzuri wa teknolojia isiyo na gharama kubwa na inayoweza kutumika Tanzania nzima. Tunawasihi muitunze na muitumie kama ilivyokusudiwa,” alisema Jong.
Akielezea hatua za matumizi ya kifaa hicho alisema ni lazima kuunganisha bomba (spring tap) kwenye dumu badala ya kifuniko chake cha kawaida ambayo itaruhusu maji kutoka kwenye dumu kwenda kwenye kifaa cha kuchuja.
Aidha aliekeza kulaza dumu chini au pembeni ili kufanya maji yatiririke kwa nguvu kupitia bomba na kuingia kwenye kifaa cha kusafisha maji na kuruhusu kuaanza kutoka taratibu.
Miongoni mwa mwananchi aliepata kifaa hicho Mohammed Said Mohammed mkaazi wa Chukwani buyu alishukuru na kueleza kuwa kifaa hicho kinaweza kuwa suluhisho la upatikanaji wa maji safi Kwa urahisi.
Naye Fatma Rashid Juma Diwani wadi ya chukwani alisema utoaji wa vifaa hivyo unaenda kuakisi maono ya Serikali na ilani ya Chama cha Mapinduzi inayosisitiza upatikanaji wa maji safi na salama Ili kuimarisha afya za wananchi wote.
Jumla ya wananchi 300 kutoka wadi ya kiembesamaki, chukwani na Mbweni walinufaika na vifaa hivyo.



0 Comments