6/recent/ticker-posts

SMZ itaendeleza uhusiano uliopo kati ya Serikali ya Japan na Zanzibar uliodumu kwa muda mrefu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Balozi wa Japan nchini Tanzania Balozi Yoichi Mikami,  aliyefika Ofisini kwake Vuga Zanzibar kwa ajili ya Kufanya mazungumzo yaliyolenga kuimarisha zaidi uhusiano katika ya Zanzibar na Japan.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano ulipo  kati ya Serikali ya Japan na Zanzibar uliodumu kwa muda mrefu.

Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania Bwana Yoichi Mikami Afisini kwake Vuga Zanzibar.

Amesema uhusiano uliopo kati ya Tanzania  na Japan utaendelea kukuza mashirikiano katika pande zote mbili katika kuimarisha sekta za  Kilimo, biashara,  Maji safi na salama, maendeleo ya viwanda, utalii na miundombinu mbali mbali.

Mhe. Hemed amesema  Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inaikaribisha serikali ya japan katika kutumia fursa zilizopo katika  uwekezaji hasa katika sekta ya utalii, uchumi wa buluu, Kilimo na matumizi ya teknolojia kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.

Aidha, Mhe. Hemed amesema Japan imepiga hatua kubwa katika masuala ya kilimo na biashara kutokana na kuwa na wataalamu wa fani mbali mbali , nyenzo  na teknolojia.

Hata hivyo, Amemuhakikishia Balozi Mikami kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana  na Serikali ya Japan  katika sekta mbali mbali hasa katika Sekta za kimkakati zinazolenga kuimarisha Diplomasia ya kiuchumi.

Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Tanzania Bwana Yoichi Mikami ameipongeza serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa  kupiga hatua katika Nyanja za kiuchumi na kijamii na kwamba ameahidi kuendeleza ushirikiano ulipo kati ya Tanzania na japan.

Balozi Mikami ameahidi kuwa  Japan itaendeleza uhusiano uliopo wa pande zote mbi kwa maslahi mapana ya wananchi wa pande zote mbili.

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe  10 / 02 / 2026.

Post a Comment

0 Comments