MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepunguza kwa kiwango kikubwa ada za usajili wa vyombo vya habari mtandaoni, hatua iliyoleta afua kwa wana habari wa mitandao na kulenga kuwezesha wamiliki wa blogu, Online TV na majukwaa ya kidijitali kufanya kazi zao kwa urahisi na gharama nafuu.
Maboresho hayo ya ada ya leseni kwa vyombo vya habari mtandaoni imepunguzwa kutoka Shilingi laki tano (500,000/) hadi Elfu Hamsini (50,000), huku ada ya maombi ya leseni ikishushwa kutoka Shilingi Elfu Hamsini (50,000) hadi kufika Sh. Elfu Kumi (10,000) pekee.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji ulioandaliwa na TCRA katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, alisema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya sekta ya habari ili kuendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya jamii.
Mwinjuma pia ameiagiza TCRA kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha madai ya mishahara na stahiki za wafanyakazi wa vyombo vya habari yanashughulikiwa kwa haraka, akisisitiza kuwa ndani ya wiki moja anatarajia kupokea taarifa ya hatua zilizochukuliwa.
Amesema Serikali itaendelea kulinda haki ya wananchi kupata taarifa, huku akihimiza vyombo vya habari kuzingatia maadili ya taaluma, kuongeza ubora wa maudhui na kulinda haki miliki.
“Vyombo vya habari vina wajibu wa kuwafikia wananchi wote bila ubaguzi, hususan waliopo vijijini, na kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Unde (AI) kwa kuongeza tija,” alisema Mwinjuma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Watangazaji Huru Tanzania (NIBA), Amos Ngosha, aliomba Serikali kupunguza idadi ya tozo zinazotozwa sekta ya utangazaji, akieleza kuwa vyombo vya habari hulipa zaidi ya tozo 19 kwa mwaka, hali inayopunguza uwezo wao wa kifedha na uendelevu wa huduma.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari, alisema mwaka 2025 jumla ya wanahabari zaidi ya 2,000 walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo, huku usikivu wa redio nchini ukifikia asilimia 85 na usambazaji wa televisheni kupitia satelaiti kufikia asilimia 100.
Ameongeza kuwa hadi Desemba 2025, leseni 770 za utangazaji zilikuwa zimetolewa, na kwamba TCRA ina mpango wa kuanzisha mfumo wa redio ya kidijitali ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano.
Mkutano wa siku mbili unaofanyika Februari 12 na 13, 2026, umewakutanisha viongozi na wadau wa sekta ya utangazaji kujadili mikakati ya kuimarisha na kupanua huduma za habari nchini.



0 Comments