6/recent/ticker-posts

Uzinduzi wa Kambi ya Uchunguzi wa Afya Viwanja vya Amani Complex



Mkurugenzi wa Tiba katika Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Msafiri Marijani, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya
Dkt. Marijani ameyasema hayo katika Viwanja vya Amani Complex wakati akizindua Kambi ya Uchunguzi wa Afya kwa maradhi mbalimbali iliyoanza tarehe 3 Februari, 2026

Amesema kambi hiyo imelenga zaidi maradhi yasiyoambukiza pamoja na maradhi mengine, akieleza kuwa mwenendo wa magonjwa umebadilika kutokana na mtindo wa maisha wa sasa hali inayosababisha kuongezeka kwa maradhi hayo duniani kote

Ameeleza kuwa uanzishwaji wa kambi za uchunguzi wa afya unalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma bora kwa urahisi na kuwaondolea usumbufu wa kufuata huduma hizo katika vituo vya afya vya mbali

Dkt. Marijani ameongeza kuwa maradhi mengi yasiyoambukiza hayana dalili za awali, hali inayosababisha gharama kubwa za matibabu pindi yanapogundulika yakiwa yamekomaa, hivyo Serikali imeamua kuanzisha kambi hizo ili kuyagundua mapema na kupunguza gharama za matibabu.

Amesema magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu husababisha ugonjwa wa moyo, jambo linalohatarisha maisha ya wananchi, na kusisitiza kuwa uchunguzi wa mapema utasaidia kupunguza kasi ya magonjwa hayo.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Juliati Magandi, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, amewahimiza wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kupata huduma za afya bure zinazotolewa kupitia kambi hiyo, akieleza kuwa ni fursa adhimu kwao.

Amefafanua kuwa wananchi watakaobainika kuhitaji rufaa watachukuliwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi, ambapo watasaidiwa kupata huduma sahihi kulingana na mahitaji yao ya kiafya

Magandi ameongeza kuwa huduma hizo zinaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi, akibainisha kuwa katika siku ya kwanza pekee zaidi ya wananchi 300 walipatiwa huduma

Amesisitiza kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili itaendelea kutoa huduma kwa wananchi wote bila ubaguzi, ili kutimiza azma ya Serikali ya kuwahudumia wananchi wake ipasavyo


 

Post a Comment

0 Comments