NA IMANI MTUMWA 05/02/2026
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mohd Ali Abdalla amesema Idadi ya ajali za barabarani zimeongezeka hadi kufikia 80 sawa na asilimia 6.2 kwa mwaka 2025 ukilinganisha na mwaka 2024 ziliripotiwa idadi ya ajali 75.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbali mbali huko Ofisini kwake Vuga Wilaya ya Mjini Amesema ajali hizo zimesababisha vifo visivyopungua 74 kwa mwaka 2025 ambapo kwa mwaka huu 2026 ulioanza tayari vimeripotiwa vifo 5 hali inayosababisha athiri kubwa katika jamii.
Aidha ameeleza kuwa ajali hizo zinatokana na uchakavu wa vyombo vya moto, uzembe wa madereva wazembe na watembea kwa miguu,kutofuata kanuni na sheria za barabarani kwa madereva na watembea kwa miguu pamoja na ongezeko la vyombo vya moto na utoaji holela wa leseni kwa baadhi ya maeneo.
“Kuna baadhi ya gari kwasiku inapigwa faini mara 5 hiyo inaonyesha haichukuliwi tahadhari na kutotii sheria za barabarani hivyo mamlaka ya usafiri barabarani inapaswa kuichukulia hatua gari kama hiyo sambamba na kuzitaka boda boda zote zilizokua hazijasajiliwa kusitishwa kuchukua abiria”, ameeleza Mkuu wa Mkoa huyo.
Aidha amefahamisha kuwa kutokuwa makini kwa baadhi ya madereva ambao hutumia barabara vibaya kwa kutopita katika vyuo vinavyotoa elimu ya udereva na kutotoa holela hivyo amezitaka taasisi husika kufuata Sheria zinazostahiki kwa kuepusha ajali na vifo vya mara kwa mara
Hata hivyo ameomba mamlaka husika kuchukua tahadhari kwa kuandaa operesheni zitakazohusisha askari wa usalama barabarani kwa kuchukua hatua stahiki na kuacha muhali ili kila moja apewe adhabu stahiki kwa mujibu wa sheria
Mkuu wa Mkoa huyo ameisisitiza Mamlaka ya Leseni na Usalama Barabarani kuchukua hatua kwa madereva ambao watakaorejea makosa kila mara kuwafutiwa usajili leseni za madereva wanaofanya hivyo ili kuweza kuokoa maisha ya watu na mali zao
Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi Bakar Suleiman Juma amesema Jeshi la Polisi limeanzisha mfumo wa kudhibiti ajali za barabarani kwa kuanzisha operesheni ya kukamata madereva wazembe na waendao mwendo kasi kuanzia tarehe 4 Febuari mwaka huu.
“Katika operesheni hiyo tayari tumekamata gari 19, bajaji 2 na pikipiki 18 na kila dereva amekamatwa na kuwekwa ndani na kila mmiliki wa gari na yeye anawekwa ndani na kuchukuliwa hatua za kisheria na kati ya hao madereva 26 hawana leseni ya njia”, amefahamisha Mkuu huyo wa Operesheni.
Aidha amewataka madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kufuata Sheria zilizowekwa barabarani ili kuepusha ajali za mara kwa mara na kupunguza vifo na majeruhi.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri barabarani Mkadam Khamis Mkadam amesema wameanzisha uhamasishaji wa kufuata Sheria na utoaji wa elimu kwa viongozi wa dini wa Mikoa yote ya Unguja na Pemba kwa kuwataka kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yao kuhakikisha suala la ajali za barabarani linapungua nchini.
.jpeg)
.jpeg)

0 Comments