Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akipokea kutoka kwa Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar hundi ya shilingi bilioni 200 ambazo ni ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya mitaji ya kuwawezesha vijana na wanawake, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Februari 05, 2026. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amekabidhi hundi ya shilingi bilioni 200 kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka ikiwa ni utekelezaji wa vitendo wa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ya kutenga na kutoa mitaji kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake.
Pia, Waziri Mkuu amesema uwezeshaji wananchi kiuchumi ni mhimili wa kukuza uzalishaji, biashara, uwekezaji na ustawi wa maisha ya wananchi, hasa vijana na wanawake ambapo amezitaka wizara, taasisi na mamlaka za kisekta zinazoendelea kutekeleza mpango huo kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa wote na program zilizokusudiwa na kutoa tija tarajiwa.
“Utoaji wa Hundi ya Shilingi Bilioni 200 unaonesha kwa vitendo kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza ahadi zake kwa vitendo, si kwa maneno. Tukio hili linaweka msingi mpya wa kuimarisha ushiriki wa vijana na wanawake katika uchumi wa Taifa na kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi jumuishi na endelevu.”
Amekabidhi hundi hiyo leo Alhamisi, Februari 5, 2026 katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza kuwa mafanikio hayo hayatapimwa kwa kiasi cha fedha kilichotolewa, bali kwa mabadiliko halisi ya maisha ya wananchi, hususan vijana na wanawake.
“Wizara, Taasisi na Mamlaka zote zinazoshiriki katika utekelezaji wa uwezeshaji kiuchumi lazima zibadilishe mtazamo kutoka katika kutoa fedha kwenda katika kusimamia matokeo na kwamba kila taasisi ijiwekee malengo yanayopimika, viashiria vya utendaji na ratiba za utekelezaji, ili kuhakikisha mitaji hiyo inazalisha ajira, kipato na biashara endelevu.”
Waziri Mkuu amesisitiza kwamba uwezeshaji huo usiwe zoezi la kawaida la kiofisi bali uwe chombo cha mageuzi ya kiuchumi, hivyo utekelezaji wa Shilingi Bilioni 200 lazima uendeshwe kwa uwazi na uwajibikaji. “Taarifa za maendeleo zitolewe mara kwa mara, na hatua zichukuliwe dhidi ya matumizi mabaya. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka dhamira ya uwezeshaji huu.”
Kadhalika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema katika kipindi kifupi cha Novemba 2024 hadi Januari 2025, Serikali kupitia mifuko na programu za kuwawezesha wananchi kuichumi imetoa mikopo na dhamana zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 66.9 kwa wanufaika zaidi ya 13,000, wakiwemo vijana na wanawake katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu); William Lukuvi amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa kinara katika kukuza uwezeshaji kiuchumi pamoja na jitihada mbalimbali anazofanya katika kuhakikisha vijana na wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha mitaji.
Waziri Lukuvi amesema hata hivyo, changamoto ya upatikanaji wa mitaji ikiwemo mikopo, vifaa, mashine na mitambo bado imekuwa kikwazo kikubwa cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi zinazotekelezwa na vijana na wanawake. ”Kutokana na changamoto hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza fedha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake.
Amesema uwezeshaji huo wa shilingi bilioni 200 ni uthibitisho wa maono na dhamira aliyonayo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inayolenga kupanua wigo wa upatikanaji wa mitaji ya gharama nafuu kwa vijana na wanawake ili waweze kuwa shindani kitaifa, kikanda na kimataifa.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka, Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar (kulia) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) William Lukuvi (kushoto), wakati wa hafla ya makabidhiano ya hundi ya shilingi bilioni 200 ambazo ni ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya mitaji ya kuwawezesha vijana na wanawake, katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Februari 05, 2026. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 Comments