6/recent/ticker-posts

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Mwigulu Nchemba Azindua Ujenzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Mwigulu Nchemba, akipanda mti katika eneo la Chuo Kikuu Mzumbe kampasi ya Tanga mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo hicho 
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, leo tarehe  15 Februari, 2026 akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa miundombinu ya Chuo Kikuu Mzumbe kampasi ya Tanga ambayo hadi kukamilika kwake utagharimu  zaidi ya shilingi bilioni 12. Pembeni yake ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wanu Hafidh Ameir.
Muonekano wa Chuo Kikuu Mzumbe kampasi ya Tanga ambayo hadi kukamilika kwake utagharimu  zaidi ya shilingi bilioni 12 ambao umewekwa jiwe la msingi na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, akizungumza na wananchi wa Tanga mjini mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa miundombinu ya Chuo Kikuu Mzumbe kampasi ya Tanga ambayo hadi kukamilika kwake utagharimu  zaidi ya shilingi bilioni 12 leo tarehe 15 Februari, 2026. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU.

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa miundombinu ya Chuo Kikuu Mzumbe kampasi ya Tanga ambayo hadi kukamilika kwake utagharimu  zaidi ya shilingi bilioni 12.

Akizungumza baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo, uliopo kata ya Gombero, Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, ambao unafadhiliwa na benki ya Dunia kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa ujenzi wa aina hiyo ya mradi unaleta heshima na kutoa uhuru wa nchi. “Mradi huu umetekelezwa kwa ubora na thamani ya fedha inaonekana”

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipambanua kwa kuacha alama kwenye maisha ya Watanzania kwa kutekeleza miradi inayogusa wananchi moja kwa moja.

Kadhalika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameihakikishia Benki ya Dunia kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa benki hiyo wakati wote.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wanu Hafidh Ameir amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya Taifa. “Tunamshukuru pia kwa uongozi wake thabiti, maono na dhamira ya dhati ya kuifanya elimu ya juu kuwa nyenzo ya mageuzi ya kiuchumi”

Amesema kupitia mradi huo Serikali imedhamiria kubadilisha taswira ya elimu ya juu nchini kwa kusogeza  huduma hiyo karibu zaidi na wananchi. “Wizara itaendelea kusimamia miradi ya HEET kwa kuzingatia thamani ya fedha, ubora na muda uliopangwa huku ikiimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ili iweze kuwa na tija.

Miradi inayoendelea kutekelezwa kupitia mpango huo ni ujenzi wa jengo la taaluma lenye jumla ya madarasa sita, maktaba ndogo, Ukumbi wa mihadhara, maabara mbili zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kila moja, pamoja na ofisi 36 zitakazohudumia wafanyakazi 72.

Aidha majengo mengine ni Hosteli mbili za wanafunzi, bwalo la chakula, kituo cha afya kitakachohudumia wanafunzi, wafanyakazi na wananchi wa vijiji vilivyopo jirani na chuo, nyumba 4 za wafanyakazi, mfumo ya majitaka na dampo la kuhifadhia taka ngumu pamoja na tenki la kuhifadhi maji safi la ujazo wa lita 400,000.

Hadi kufikia Februari 13, 2026 ujenzi wa kampasi hiyo ulikuwa umefikia asilimia 82.

Post a Comment

0 Comments