6/recent/ticker-posts

Serikali imefanikiwa kudumisha amani, utulivu na mshikamano kwa wananchi wa Zanzibar -Mhe.Kitwana

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa amesema Serikali imefanikiwa kudumisha amani, utulivu na mshikamano kwa wananchi wa Zanzibar kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Rahaleo Zanzibar kuhusu Siku 100 za Mafanikio ya Uongozi wa Dkt. Mwinyi 

Amesema kuwa ni waajibu  kwa wananchi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wanasimamia, kuilinda na kuidumisha amani ya nchi, kwani amani na utulivu ni msingi wa maendeleo katika jamii,  amani itakapovunjika hakutakuwa na ustawi wa maendeleo katika nchi.

Waziri Kitwana amefahamisha kuwa Serikali inaendeleza mradi wa Ujenzi wa Ofisi za Masheha ambapo jumla ya ofisi 48  zimejengwa na ujenzi wake  umefikia asilimia 50 kati ya ofisi hizo, 28 zimejengwa Unguja na 20 zimejengwa Pemba. 

"Ofisi imekamilisha maandalizi ya ujenzi wa Ofisi tano (5) za Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Ofisi 11 za Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na Ofisi mbili (2) za Wilaya ndogo za Tumbatu na Kojani, Ofisi hizi zote nilizozitaja zinatarajiwa kujengwa katika mwaka wa fedha 2026/2027" ameeleza.

Akizungumzia kuhusu kuimarisha usafi wa miji, amesema Serikali imefanikiwa kuwakabidhi wakandarasi maeneo 111 ya ujenzi wa Vituo vya kukusanyia taka ambapo kati ya vituo hivyo, 73 vitajengwa Unguja na Vituo 38 vitajengwa Pemba.

Aidha ameeleza kuwa Serikali imefunga mkataba wa kununua gari 29 ya kuchukulia taka ambapo gari mbili zimeshawasili na gari 27 zitawasili nchini ifikapo mwezi Mei, 2026.

Mhe. Kitwana amesema kuwa Serikali imeingia mkataba na Kampuni  Binafsi  kuliendesha Jaa Kuu la Kibele pamoja na kuzalisha nishati mbadala inayotokana na taka katika Jaa hilo sambamba na kufanya mazungumzo na Kampuni mbali mbali  za nje ya Nchi, zenye uwezo wa kutoa huduma za usafi wa Miji pamoja kupendezesha Miji na kuwa katika mandhari nzuri.

Amesema kuwa Serikali imekamilisha ujenzi wa masoko ya Mombasa, Kitope, Kengeja na Mzambarauni ambapo soko la Mombasa na Kitope tayari yameanza kutowa huduma na kwa upande wa soko la Kengeja na Mzambarauni hatua za mwisho zinakamilishwa ili kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii amesema Wizara imejenga jengo la kisasa la Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Wilaya ya Kaskazini “B” katika eneo la Mahonda ambapo ujenzi huu ulianza mwezi Novemba 2025 na sasa ujenzi umefikia   asilimia 45.

Hata hivyo amefahamisha kuwa serikali imeimarisha mifumo ya usajili wa matukio ya kijamii ikiwemo vizazi, vifo, ndoa na talaka ambapo mifumo hiyo imesaidia kupunguza muda wa upatikanaji wa vyeti pamoja na kusaidia kusoma taarifa za mifumo mengine ya taasisi nchini. 

Ameeleza kuwa katika kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanikiwa  kuboresha mazingira ya kazi na makaazi ambapo Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) kimefanikiwa kujenga mahanga 15 kwa ajili ya makaazi ya maafisa na wapiganaji wa kikosi hicho.

"KVZ kimefanikiwa kuendeleza ujenzi wa majengo mawili ya Hospitali yenye hadhi ya Hospitali za Wilaya katika Kambi ya Makao Makuu Mtoni na Kambi ya Ndugu Kitu Pemba" amefahamisha.

Sambamba na hayo ameeleza kuwa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) limeendeleza ujenzi wa mahanga ya ghorofa mbili yenye jumla ya nyumba 30 kwa ajili ya maafisa na wapiganaji katika Kambi ya Ng’ambwa Pemba ambapo Wakala wa Ulinzi JKU imejenga jengo la Makao yake  lenye ghorofa mbili katika eneo la Mtoni. 

Amesema kuwa Serikali imeboresha mafunzo ya utendaji kazi ambapo jumla ya maafisa na wapiganaji 1,375 wa Idara Maalum za SMZ wamepatiwa mafunzo yanayoendana na tekinolojia na mifumo ya intelijensia ya kisasa katika vyuo vya ndani na nje ya nchi. 

Aidha amefafanua kuwa Serikali imeimarisha mradi wa kuimarisha ulinzi na usalama Zanzibar kwa kuhakikisha imefunga mifumo ya kisasa ya mawasiliano ya ulinzi katika  Idara  maalum za SMZ, upatikanaji wa vitendea kazi zikiwemo sare za maafisa na askari pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ya kamera za usalama (CCTV) katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.







 

Post a Comment

0 Comments