6/recent/ticker-posts

TPF-Net SONGWE WAMFARIJI MKE NA ASKARI ALIYEPATA ULEMAVU WA KUDUMU.

Na Issa Mwadangala.

Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Songwe (TPF-Net) kwa kushirikiana na wanawake kutoka Majeshi mengine Mkoani humo wamemtembelea Konstebo wa Polisi Haluna Komba aliyepata ajali akiwa kazini na kusababisha ulemavu wa kudumu, na kumpa faraja pamoja na mahitaji mbalimbali ya msingi ikiwa ni ishara ya upendo na mshikamano kwa askari mwenzao anayekabiliwa na changamoto za kiafya na maisha.

Akizungumza tarehe 06 Machi 2026 alipokuwa nyumbani kwa askari huyo katika Kata ya Itumba, Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Maria Kway amesema wanawake wa Majeshi mbalimbali wameguswa na hali ya askari huyo pamoja na familia yake, hivyo wakaona ni muhimu kufika nyumbani kwake ili kumpa faraja na kuonesha kuwa hayuko peke yake katika kipindi hiki kigumu.

ACP Kway alibainisha kuwa awali askari huyo alikuwa akihudumiwa na mke wake, lakini baada ya mke wake naye kupata ajali iliyomfanya kwa sasa ashindwe kutembea, familia hiyo imejikuta ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha jambo ambalo linawafanya kumtembelea na kumfariji kila wanapopata wasaa.

ACP Kway, alisema kuwa tukio hilo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani itakayofanyika Machi 08, 2026, ambapo wanawake wa majeshi hayo wameonesha mshikamano, upendo na moyo wa kujitolea kwa kuwasaidia wenzao waliopatwa na changamoto huku wakihimiza jamii kuendeleza utamaduni wa kusaidiana wakati wa matatizo.



Post a Comment

0 Comments