Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, marehemu William Lukuvi katika Ibada ya kumuombea iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Machi 27, 2026.
Mwili wa marehemu William Lukuvi aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, ulipowasili kwenye viwanja vya Bunge kwa Ibada ya kumuombea, Machi 27, 2026.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza katika ibada ya kumuombea aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, marehemu William Lukuvi katika Ibada ya kumuombea iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Machi 27, 2026. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akiagana na Makamu wa Rais mstaafu, Dkt. Philip Mpango baada ya kuongoza waombolezaji katika Ibada ya kumuombea aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, marehemu William Lukuvi iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Machi 27, 2026. Kushoto ni Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema enzi ya uhai wake, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Isimani, Mheshimiwa William Lukuvi alikuwa mshauri kwa watu wengi wakiwemo wabunge na mawaziri.
“Mimi ni mmojawapo wa watu walionufaika na ushauri wake tangu nikiwa Naibu Waziri wa Fedha na hata sasa alipoteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu aliendelea kunishauri kwa karibu zaidi,” amesema.
“Alikuwa na kiwango cha juu cha kujitolea, atakumbukwa sana kama mshauri na mlezi wa kila mmoja, na kwa muda mrefu nimekuwa mmojawapo kati ya wengi walionufaika na busara zake.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 27, 2026) wakati akizungumza katika ibada ya kumuombea marehemu na kisha kuwaongoza viongozi wa Serikali, Wabunge na waombolezaji kutoa heshima za mwisho katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.
Amesema tabia ya kujitolea kwa muda mwingi bila kuchoka ilimpa yeye amani hata akaweza kufanya ziara ndefu ya mikoa sita mfulululizo akipita kila Wilaya na Halmashauri kwa sababu Mheshimiwa Lukuvi alikuwepo ofisini akifanya kazi kikamilifu.
Waziri Mkuu amesema: “Hakika, kifo cha mpendwa wetu Mheshimiwa Lukuvi kimetuacha Watanzania wengi wakiwa na simanzi kubwa. Mimi binafsi nimekuwa nikiwasiliana naye na kushauriana naye mara kwa mara. Hata siku ile tulipoarifiwa kwamba hali yake ya afya imebadilika, tulikuwa tukiwasiliana na kupanga shughuli mbalimbali za kazi, tukijadili vikao na ratiba za Kamati.”
“Serikali na Bunge tumeondokewa na kiongozi ambaye ataendelea kukumbukwa kwa busara zake, ukomavu wake kisiasa, weledi katika kazi, uzalendo na kiwango cha juu cha uratibu,” ameongeza.
Waziri Mkuu ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, wananchi wa Jimbo la Isimani na Watanzania wote kwa ujumla. “Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa ustahimilivu na faraja katika kipindi hiki kigumu,” amesema.
Mheshimiwa Lukuvi alifariki dunia Machi 25, 2026 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa.
Mapema, Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Philip Mpango alisema Mheshimiwa Lukuvi alikuwa akitumiwa na Serikali kuwafunda Mawaziri na kuwakumbusha wajibu wao. “Ndani ya Bunge, alipenda kuwashauri wenzake na mimi binafsi alikuwa nguzo ya kunielekeza taratibu za ndani ya Bunge,” alisema.
Naye, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mwanaasha Khamis Juma alisema amefanya kazi kwa muda mfupi na Mheshimiwa Lukuvi lakini alitambia kwamba alikuwa ni kiongozi mahiri aliyependa maendeleo ya pande zote mbili za Muungano.
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Damu Azizi ya Yesu iliyopo Kisasa, Dodoma Padre Sostenes Ndyenja alisema wanafamilia, viongozi wananchi na waombolezaji waliokuwepo kwenye ibada hiyo wanapaswa kumshukuru Mama aliyemzaa na kumpa elimu Waziri Lukuvi.
“Alikuwa kama ua zuri lemye harufu nzuri kwa sababu ya yale aliyoyatenda. Kuna maua mengine huwa yana harufu mbaya, hayapendwi. Lakini Waziri Lukuvi alikuwa ni ua zuri lakini ghafla amenyauka. Kipindi ukiwa umechanua, unaangaza kwa watu wengine.”
Akitoa mfano wa kufufuliwa kwa Lazaro aliyekuwa ananuka, aliwataka wanadamu waache tabia ya kuona mabaya ya wenzao kama ndiyo habari za kuzitangaza huko na huko. “Tuache kuwa mabalozi wa kutangaza mabaya ya wenzetu, tujiulize na sisi baada ya maisha yetu tutaweza kuelezewa kwa namna gani?”
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
IJUMAA, MACHI 27, 2026.
0 Comments