Na Maelezo Zanzibar 12.03.2026
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha sekta zilizopo chini ya Wizara hiyo kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, ubunifu na matokeo yenye tija kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo kuhusu siku 100 za mafanikio ya uongozi wa awamu ya pili ya Dkt. Mwinyi amesema Wizara imejikita katika kuimarisha mawasiliano ya Serikali kwa kukuza sanaa na utamaduni wa kizalendo, kuendeleza michezo ikiwa ni ajira na afya kwa jamii.
Amesema kuwa kupitia utekelezaji wa mipango ya maendeleo yameleta mafanikio mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa ubora wa huduma za habari, kuimarika kwa usimamizi wa shughuli za sanaa na utamaduni, pamoja na kuendeleza miradi ya kimkakati inayolenga kukuza uchumi wa ubunifu ili kuibua vipaji.
Akizungumzia sekta ya habari Dkt. Riziki amesema Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) limeboreshwa na kupatiwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya uzalishaji na urushaji matangazo hatua inayoongeza ubora wa huduma za habari pamoja na kusajiliwa na kuwapatia vitambulisho (Press cards) waandishi wa habari 570 ili kuimarisha uwajibikaji na weledi katika kazi za uandishi wa habari.
“Taasisi hiyo imepata vifaa vya kisasa ikiwemo kamera, kompyuta mpakato na mitambo ya kurushia matangazo kwa vituo vya Unguja, Pemba, Dodoma na Dar es Salaam ili kuongeza ubora wa picha na sauti katika matangazo na kuongeza ushindani wa ZBC na vyombo vingine vya habari nchini” ameeleza Dkt. Riziki.
Aidha amesema kupitia Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari, Wizara imefanikiwa kuhifadhi utamaduni pamoja na kuvutia utalii kwa kuonesha ngoma, mavazi na vyakula vya asili vya Zanzibar ambalo limechangia kukuza Uchumi.
Amefahamisha kuwa katika kuendeleza miundombinu ya michezo, Serikali inaendelea kusimamia ujenzi wa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa mji wa michezo wa AFCON City unaojengwa Fumba wenye thamani ya dola milioni 150, ambao hadi sasa umefikia asilimia 35 ya utekelezaji wake.
“Ujenzi wa viwanja vya michezo katika wilaya na mikoa mbalimbali umefikia zaidi ya asilimia 90, huku viwanja 13 tayari vimekamilika” amesema Waziri.
.jpeg)
0 Comments