Na Ameir Khalid
WIKI moja imepita tangu timu zetu za Zanzibar zilizokuwa zikishiriki michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika 'CAF' zitolewe katika mashindano hayo kwa kupoteza mechi zao za ugenini.
Mabingwa wa soka humu visiwani Zanzibar Ocean View iliyokuwa ikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa, ilitolewe na klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kuchapwa magoli 3-0, huku makamo bingwa KMKM wakitupwa nje na DC Motema Pembe pia ya DRC kwenye Kombe la Shirikisho kwa kipigo cha magoli 4-0.
Napenda kuzipongeza klabu zetu hizo kwa kuweza kufikia hatua ya angalau kushiriki mashindano makubwa kama hayo, ingawa kutolewa kwao katika hatua za mwanzo, ni jambo linaloibua masuala mengi ndani ya mawazo yangu na pengine ya wapenda soka wote nchini.
Ninavyojiuliza ni je, kutolewa mapema hivyo, ni matokeo ya maandalizi mabovu, kiwango kidogo cha timu zetu, kukosekana ligi yenye upinzani au kutokuwa na uzoefu wa michezo ya kimataifa?
Kwa masuala haya, ninaamini kuwa kila mtu atakuwa na majibu yake, ambayo mengine yatalingana na yapo yatakayotafautiana.
Lakini kwa upande wangu, nina imani kuwa kilichowaangusha wawakilishi wetu hawa ni mambo mawili ambayo kwa sasa ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayovisumbua visiwa vyetu katika jitihada za kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu.
Sababu ya kwanza ni kutokuwa na maandalizi mazuri katika kuziandaa timu kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo, ambayo kwa hakika yalihitaji kujengewa mikakati madhubuti na maandalizi ya muda mrefu na yaliyo mazuri sambamba na mechi za kirafiki.
Ni jambo linalofahamika kuwa kila aina ya mashindano inakuwa na kiwango chake cha maandalizi, na timu haiwezi kujiandaa kwa michuano ya klabu bingwa Afrika, kwa kujipima nguvu na timu za nyumbani tena baadhi yao za daraja la pili au la kwanza kanda.
Kufanya hivyo ni sawa na kufanya mazoezi ya kukimbia mita 100 au 200 wakati mtu akitarajia kushindana katika mbio za mita 1,500 au zaidi ya hapo, huku akiwa na imani ya kushinda.
Sababu nyengine ya kuboronga kwa timu zetu katika mashindano ya kimataifa ni kutokuwa na ligi nzuri na yenye msisimko hapa nchini, ambayo ingechangia kuziimarisha timu zetu na kuziweka vyema kabla kuingiza mguu viwanjani kusaka mataji makubwa.
Ligi yenye ushindani wa kweli na usiojali uwezo wa baadhi ya timu kifedha ndiyo yenye kuzalisha wawakilishi wazuri katika soka la kimataifa.
Hebu tujiulize mwaka 1997 wakati klabu ya Mlandege ilipofika fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati na kutolewa na Rayon Sport ya Rwanda, ilikuwa na mganga gani ambaye sasa amekufa?
Aidha Simba ya Dar es Salaam, imekuwa ikifanya vizuri na hata kufika fainali za michuano ya Afrika, je, palikuwa na mganga?
Ninachokiona kuwa kilichangia mafanikio yale, ni maandalizi mazuri na yasiyokuwa ya zimamoto, na pia ligi iliyoendeshwa bila mizengwe kama ilivyo sasa.
Sidhani kama wapo wanaofurahia mwenendo huu wa timu zetu hasa linapokuja suala la mashindano ya kimataifa.
Kila mmoja anafahamu kuwa Zanzibar imejaaliwa vipaji vya hali ya juu kisoka vinavyohitaji kuendelezwa tu, lakini kinachowashangaza wengi, ni kuona vipaji hivyo havisaidii kuziletea mafanikio timu zetu.
Kichekesho ni pale unapofika wakati wa kuingia mashindanoni, tunaposikia viongozi na makocha wa timu wakijigamba kwa sauti za juu kwenye maikrofoni za redio na televisheni, kuwa wameziandaa vizuri timu zao na kwamba ushindi hauna shaka.
Kwa upande mwengine, tabia ya kuwadekeza waamuzi wanaofanya kazi kwa utashi na maslahi binafsi kwa kuzibeba baadhi ya timu, nako kunachangia kuporomosha soka letu na hivyo kutukosesha wawakilishi walio bora.
Hili la kuzishindisha timu kutokana na uwezo wao wa kifedha badala ya ufundi wa soka, haliwezi kutufikisha kileleni mwa ufanisi na badala yake litavuruga ligi zetu na kujenga ukuta kati ya chama kinachosimamia soka, wenye timu na mashabiki wao.
Pamoja na uzalendo nilionao na kutaka timu zetu zifanye vyema, lakini ningeshangaa kama wawakilishi wetu wangeshinda na kusonga mbele katika michuano ya Afrika, kwani hatua hiyo ingekuwa sawa na ngamia kupenya katika tundu ya shindano.
Jitihada zinahitajika ili Zanzibar irudi katika zile zama za soka la kuvutia na litalomfanya kila mtu ajisikie vibaya kukosa mechi ya ligi.
Wachezaji wa kizazi hichi waone aibu kusimuliwa tu kwamba walikuwepo akina Shioni Mzee, Salum Mkweche, Abdulmajham Omar, Mzee Mwinyi, Nassor Mashoto, Suleiman Nyanga, Maulid Machaprala na wengine wengi.
Simulizi hizo ziwe chachu na changamoto kwao ya kujituma na kutaka kufikia walipofika wenzao ili vizazi vijavyo navyo vipate kuwaandika na kuwaambia watoto wao kuwa walikuwepo akina fulani na fulani.
No comments:
Post a Comment