Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi Mipango, Wakurugenzi Utumishi wa Mawizara na Taasisi zote za Umma kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi Mipango, Wakurugenzi Utumishi wa Mawizara na Taasisi zote za Umma kufanya kazi kwa kushirikiana na kufuata sheria, kanuni na miongozo ya Utumishi Serikalini ili kuweza kufikia malengo ya Serikali iliyojiwekea.
Ameyasema hayo kwenye kikao kazi kilichowakutanisha Viongozi wa ngazi mbali mbali Wakuu wa Taasisi na Wakurugenzi kilichofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Amesema katika kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa jamii ni lazima wakuu wa Taasisi na wakurugenzi kufanya kazi kwa kufuata sheria hasa katika utoaji wa maamuzi na kuepuka kuzitumia vibaya dhamana zao kama silaha za kuwaumiza watendaji walio chini yao.
Mhe. Hemed amewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanapanga mipango yenye kulenga katika maono ya Serikali na kuachana na matumizi mabaya ya fedha za Serikali yasiyo na tija kwa Taifa na badala yake wabuni vyanzo mba mbali vya ukusanyaji wa mapato vitakavyosaidia kusukuma mbele maendeleo ya Zanzibar.
Katika kufikia adhma na malengo ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi ya kuwaletea maendeleo kwa Wazanzibari, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka viongozi kuzitumia vyema rasilimali za nchi ili kuweza kufanya kazi na kutoa huduma kwa uweledi na ufanisi mkubwa jambo litakalowapa Imani wananchi kwa Serikali yao.
Amewataka Wakurugenzi Utumishi kuangalia kwa umakini haki na maslahi ya watumishi pamoja na kuimarisha Mifumo ya utowaji na upatikanaji wa huduma ili kuepusha changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na malalamiko yatolewayo na watumishi hasa wakati wanapostaafu kazi.
Amesisitiza suala la nidhamu kwa watumishi wa Umma, uwajibikaji, na kufuata taaratibu za kazi na kuagiza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa watumishi watakaokwenda kinyume na taratibu za Utumishi Serikalini.
Kwa upande wake katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Muhandizi Zena Ahmed Said amewataka viongozi hao kusimamia haki na usawa kwa watendaji wao na kujiepusha kuwa chanzo cha migogoro, mifarakano na kuwagawa watu makundi jambo linalopelekea kuzorota kwa ufanisi wa kazi.
Mhandisi Zena amefahamisha kuwa kila mtendaji wa serikali ana wajibu wa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa kwa kuzingatia wakati, ubora na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amewaasa viongozi hao kuacha kufanya matendo yote yaliyokatazwa katika Sheria na kanuni za Utumishi wa Umma ambayo yatawashushia hadhi wao binafsi na serikali kwa ujumla sambamba na kuepuka kutumia rasilimali za Ofisi kwa maslahi binafsi. 
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe 02 / 12 / 2025.


0 Comments