Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameyakaribisha makampuni na wawekezaji kutoka nchini Ufaransa kuja kuwekeza Zanzibar, hususan katika sekta kuu za uchumi ikiwemo utalii, akieleza kuwa Zanzibar iko tayari kupokea uwekezaji wenye tija na endelevu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 27 Februari 2026, Ikulu, Zanzibar, alipokutana na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Bi. Anne Sophie, aliyefika kwa mazungumzo ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Zanzibar na Ufaransa.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji wawekezaji makini na wenye mitaji ya kutosha watakaowekeza katika sekta hizo ili kuimarisha nguvu kazi, kuongeza utaalamu na kuboresha utoaji wa huduma, hususan katika sekta ya utalii na maendeleo ya uchumi wa buluu.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha sera bora za uwekezaji pamoja na kuendeleza miundombinu ya barabara na bandari, ikiwemo Bandari Jumuishi ya Mangapwani, ambayo itakapokamilika itatoa fursa pana za uwekezaji.
Amesisitiza kuhusu mkakati wa kukifungua Kisiwa cha Pemba kuwa kituo cha uwekezaji na utalii endelevu.
Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia Ufaransa kuwa Zanzibar itaendelea kuendeleza mikakati ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi, na amewasisitiza wawekezaji kutoka Ufaransa kuja Zanzibar kujionea na kubaini fursa zilizopo.
Naye Balozi Anne Sophie ameihakikishia Zanzibar kuwa Ufaransa itaendelea kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa katika kuimarisha maeneo muhimu ya kiuchumi, hususan miradi ya sekta za utalii, afya, elimu, utamaduni, uendelezaji wa Mji Mkongwe, mazingira na uchumi wa buluu




0 Comments