6/recent/ticker-posts

Wakaazi wa Nyumba za Kikwajuni waridhia kupisha ujenzi mpya wa nyumba za kisasa

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mohd Abdalla Ali akizungumza na Wakaazi wa Kikwajuni katika Mkutano wa  kukabidhi Nyumba hizo kwa ajili ya Ujenzi Mpya na kuahidiwa kurudi katika Nyumba zao baada ya kumalizika kwa Ujenzi huo ambao Unatarajiwa kuanza kwa hatua ya Ubomowaji 26/03/2026 Zanzibar.
-Baadhi ya Nyumba za Kikwajuni zinazotarajiwa Kuvunjwa na Kujengwa Upya kama zinavyoonekana .
Baadhi ya Wakaazi wa Kikwajuni wakiwa katika Mkutano na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mohd Abdalla Ali pamoja na Shirika la Nyumba ili  kukabidhi Nyumba hizo kwa ajili ya Ujenzi Mpya na kuahidiwa kurudi katika Nyumba zao baada ya kumalizika kwa Ujenzi huo ambao Unatarajiwa kuanza kwa hatua ya Ubomowaji 26/03/2026 Zanzibar
Mkaazi wa Nyumba za Kikwajuni Omar Nassor akitoashukurani kwa Serikali kwa niaba ya Wenziwe katika Mkutano wa  kukabidhi Nyumba hizo kwa ajili ya Ujenzi Mpya na kuahidiwa kurudi katika Nyumba zao baada ya kumalizika kwa Ujenzi huo ambao Unatarajiwa kuanza kwa hatua ya Ubomowaji 26/03/2026 Zanzibar.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Sultani Said Suleiman akizungumza na Wakaazi wa Nyumba za Kikwajuni katika Mkutano wa  kukabidhi Nyumba hizo kwa ajili ya Ujenzi Mpya na kuahidiwa kurudi katika Nyumba zao baada ya kumalizika kwa Ujenzi huo ambao Unatarajiwa kuanza kwa hatua ya Ubomowaji 26/03/2026 Zanzibar.

PICHA NA YUSSUF SIMAI,MAELEZO ZANZIBAR.26/02/2026

Na Maelezo Zanzibar   26.02.2026

 

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Moh’d Ali Abdallah, amesema wananchi wa Kikwajuni wameonesha uungwana, ujasiri, hekima na busara kwa uamuzi wao kutoa maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa nyumba za makaazi, hatua itakayochochea maendeleo na kuboresha ustawi wa jamii katika eneo hilo.

 

Ameyasema hayo katika eneo la Nyumba za Mjerumani, Kikwajuni, Wilaya ya Mjini, alipokuwa akizungumza na wananchi wa eneo hilo.

 

Amesema kitendo hicho kinaashiria uzalendo na mshikamano wa hali ya juu kwa wananchi kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

 

Aidha, amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati pamoja na kwa viwango vinavyotakiwa.

 

Vilevile, amewataka wananchi wa maeneo hayo kuwa walinzi wa mali na vifaa vitakavyokuwepo katika eneo la ujenzi, ili kufanikisha kwa haraka mradi huo na kuwawezesha wananchi wa Kikwajuni kurejea katika makazi yao mapya mara baada ya utakapokamilika.

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba, Ndg. Sultan Said Suleiman, amesema wamewaelekeza wakandarasi kuhakikisha kazi zote zisizohitaji utaalamu mkubwa zinapewa kipaumbele kwa wananchi wa Kikwajuni ili nao wanufaike moja kwa moja na mradi huo unaotekelezwa katika eneo lao.

 

Aidha, amesema Makamu wa Pili wa Rais anatarajiwa kujumuika na wananchi wa Kikwajuni katika futari (iftar) ifikapo tarehe 5 Machi mwaka huu kwa lengo la kuiombea dua nchi pamoja na kuombea mradi huo umalizike kwa salama na amani.


Nao wananchi wa Kikwajuni wameishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi huo, wakieleza kuwa azma ya Rais Dkt. Mwinyi ni kuwaletea maendeleo endelevu, na kuwataka wananchi wenzao kuiamini Serikali katika utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa makazi.

 

Nyumba hizo za Mjerumani zinatarajiwa kubomolewa ifikapo tarehe 26 Machi mwaka huu na ujenzi wa nyumba mpya kuanza mara moja baada ya zoezi la ubomoaji kukamilika ambapo zoezi la ullipaji wa fedha za kujikimu tayari limeanza kutekelezwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.




 

Post a Comment

0 Comments