Na Luluwa Salum - Pemba
Vyombo vya sheria nchini vimekiwa kutoa haki kwa wale wanaopatwa na majanga ya kuvunjiwa haki zao hali ambayo itasaidia kupunguwa kwa vitendo vya uzalilishaji wa wanawake nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mdhamini Wizara ya Ustawi wa Jamii ,Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto Pemba, Mauwa Rajab Makame alipokuwa akifunguwa warsha ya siku moja katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani huko katika ukumbi wa Makonyo Chake-Chake.
Alisema kuwa endapo vyombo vya sheria vitatenda haki kwa wananchi wanaopatwa na majanga ya kuvunjiwa haki zao itasaidia wananchi hao kuwa na imani na Serikali kupitia Wizara husika kwa kuona kuwa wanajaliwa na kupatiwa haki zao wanazostahiki.
Aidha aliwataka wananchi kukemea vikali ubaguzi wana uzalilishwaji dhidi ya wanawake na watoto kwa kutoa haki sawa ya elimu kwa watoto wa kike na kuwashajihisha kujikita zaidi katika masomo ya sayansi ili kuendana na Dunia ya sasa ya sayansi na Teknolojia.
Sambamba na hayo amewataka wanawake kujiendeleza katika masomo ili kuweza kushikilia nyazifa mbali mbali zinazoheshimika katika sekta rasmi za Serikali na zisizo rasmi ili kuondokana na dhana nzima ya kuwa wanawake hawawezi kuongoza katika nafasi za juu za Serikali.
Aliitumia siku hii ya wanawake Duniani kwa kuwataka wananchi kuunganisha nguvu zao pamoja kupiga vita ukimwi na kutokubali kuwaozesha watoto bila ya kupima virusi vya ukimwi ili kupunguza ongezeko la wagonjwa wa ukimwi.
Kwa upande wake mratibu wa kituo cha huduma na sheria Pemba, Hemedi Azizi Mtele alizitaja changamoto na matatizo yanayowakabili wanawake kuwa ni pamoja na ukosefu wa elimu ya sheria ujambo ambalo linasababisha kutojua haki zao za msingi kisheri kutoripoti matatizo katika vyombo vya sheria na vikwazo vinaavyowakabili wakati wa kupewa talaka na waume zao.
Nae Mkuu wa Idara ya Wanawake na watoto Pemba, Rabia Rashid Omar alisema udhalilishwaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto umekuwa ukizidi siku hadi siku nah ii ni kutokana na uwelewa mdogo juu ya haki zao kwa kuwaficha wale ambao huwafanyia udhalilishaji watoto kwa kutotoa taarifa katika vyombo husika .
Alieleza kuwa jumla ya kesi 42 za udhalilishaji wa Wanawake na watoto zimeripotiwa katika kipindi cha January hadi February 2011, ambapo kesi 6 kupigwa kwa Wanawake 24 kutelekezwa kwa Wanawake na Watoto 2 kupewa ujauzito kwa Watoto 2 kubakwa kwa Watoto 1 kutukanwa hadharani kwa Wanawake.
Maadhimisho hayo yameandaliwa na Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto Pemba, na kushirikisha Wadau kutoka Taasisi mbalimbali zinazotetea haki za Wanawake chini ya ufadhili wa Care international.
No comments:
Post a Comment