Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar
Spika wa Baraza la Wawakilishi,Pandu Ameir Kificho amesema ili kukabiliana na tishio la kutoweka kwa baadhi ya visiwa vidogo vidogo, Mataifa wanachama wamepewa changamoto ya kutunga sheria na sera ya kuvihami Visiwa hivyo.
Akifungua mkutano wa siku nne wa Wabunge wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola MjiniZanzibar jana, Kificho alisema ni lazima nchi wanachama kuchukua hatua ya kuvihami Visiwa hivyo.
“Ni lazima tuchukue hatua sasa kuvilinda Visiwa vyetu. Mabadiliko yanayotokea katika baadhi ya nchi yanaweza kufika na hata kwetu, tuwahimize watunge sera kuliona hilo katika mipango yao” Alisema Spika Kificho.
Kificho alizihimiza nchi wanachama kuchukua hatua za haraka mbali ya kutunga sheria na sera,lakini kuweka mikakati madhubuti kuviokoa Visiwa hivyo.
Mada kuu katika mkutano huo unaowashirikisha Wabunge 15 wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola wanaoishi katika Visiwa vidogo vidogo kuvihami Visiwa hivyo na tishio la mabadiliko ya tabia nchi.
Spika Kificho, amewaambia wajumbe kwamba jambo muhimu kwa sasa ni utunzaji wa mazingira sanjari na upandaji miti huku jamii ikihamasishwa katika kutoa msukumo wa uhifadhi na uendelezaji wa Visiwa hivyo.
Alisema mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi ni moja kati ya mambo yanayopewa kipaumbele na Jumuiya ya Kimataifa hivi sasa, hi vyo ni jukumu la kila nchi wanachama wa JUumuiya hiyo kujielekeza katika kutunga sheria madhubuti ya kuvilinda Visiwa na uchafuzi wa mazingira.
Akielezea ulazima wa kuvilinda Visiwa hivyo, Spika huyo alisema “Ndugu Wajumbe kuna haja Mabunge yetu kujifunza kutoka kwa Mataifa mengine yanayofanana na sisi njia bora na mikakati waliyotumia kuvihami Visiwa vyao visikubwe na janga la uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi”
Spika Kificho, ameueleza mkutano huo kuwa Zanzibar nayo imeanza kupata athari za mabadiliko ya tabia nchi ambapo katika Vijiji vilivyopo ukanda wa pwani ya Mashariki maji ya bahari yameanza kumega eneo la ardhi.
Kauli ya Spika imekuja siku moja baada ya Dk. Ali Mohmmed Shein, Rais wa Zanzibar kutembelea eneo la Viwanja vya Maisara Mjini Unguja kujionea tatizo la maji ya bahari kuathiri sehemu ya ardhi kunakosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk Willim Shija, Katibu Mkuu wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola ameuambia mkutano huo kwamba baadhi ya Visiwa vya Jumuiya hiyo vimo katika hatari kubwa ya kukubwa na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi.
No comments:
Post a Comment