Habari za Punde

WAFARANSA WAITEMBELEA IDARA YA UCHAPAJI

Na Mohamed Mzee

UJUMBE wa watu 25 kutoka Ufaransa ukiongozwa na Marc Costantini, jana ulitembelea Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Saateni kujionea hali halisi ya mitambo na namna kampuni za Ufaransa zitakavyotoa michango yao katika sekta ya uchapishaji Zanzibar.

Ukiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni , Utalii na Michezo, Abdillahi Jihad Hassan, ambaye alikuwa ndiye Mkalimani wa lugha ya Kifaransa , Constatini alieleza kufurahishwa kwake na ziara hiyo na kusema kuwa itajenga urafiki na watu wa Zanzibar.

Alisema watakuwa mabalozi wazuri wakiwakilisha kampuni zipatazo 20 za uchapishaji nchini Ufaransa na kwamba ripoti yao itasaidia kimaeneeleo.

Aidha alimshukuru Mkurugenzi wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Iddi Suleiman Suwedi na wafanyakazi wote na kusema kuwa amefarajika sana na mapokezi aliyoyapata yenye kuonesha upendo na urafiki.

Costantini na ujumbe wake waliipatia Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali shilingi 2,000,000. Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali , Iddi Suleiman Suwedi, aliushukuru ujumbe huo kwa ziara hiyo na msaada walioutoa na kuwataka kujenga ushirikiano zaidi hapa Zanzibar katika sekta hiyo ya uchapishaji.

Aidha aliwaomba kuwa mabalozi wazuri nchini mwao katika kuifikiria Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kupata uwezo wa kimitambo.

Ujumbe huo umefika hapa nchini kwa ushirikiano na kampuni ya Grand Travel International(GTI) iliyopo Shangani , mjini Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.