Habari za Punde

ZANZIBAR IMEAZIMIA KUWAPUNGUZIA UMASKINI WANANCHI- BALOZI SEIF

Na Abdulla Ali Abdulla

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi amesema kuwa kuwapunguzia umasikini wananchi, ajira kwa Vijana na kufufuwa Uchumi wa nchi ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais aliyasema hayo katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Chama cha Mabuge ya Jumuiya ya Madola (CPA) Dk. Willium Shija aliyefika Ofisini kwake kusalimiana naye.

Mheshimiwa Balozi Iddi alisema Serikali ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa imekuja kuondoa uhasama uliokuwepo miongoni mwa jamii na kuleta upendo na maelewano. Jambo ambalo limedhihirika wakati Serikli hio ilipoundwa, kwa namna viongozi wa CUF na wa CCM walivyoshirikiana katika uundaji wake.

Alisema hali ya Zanzibar ni shuwari na wanachi wanashirikiana katika kujenga nchi na kujiletea maendeleo yao. Halikadhalika Viongozi wa Serikali wanashirikiana katika utendaji bila ya kujali itikadi za vyama vyao.

Aidha, aliwasilisha Salamu za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Moh’d Shein za kufurahishwa na uwamuzi wao wa kufanya Mkutano wao hapa ambao utasaidia kuvitangaza Visiwa vya Zanzibar katika soko la Kimataifa la Utalii.

Ambapo Mhe. Balozi Iddi aliuweleza Mkutano huo kuwa utasaidia kutanabahisha athari za uchafuzi wa mazingira unaofanywa na wanaadamu ambao tayari umeshaanza kuonesha maafa katika sehemu nyingi duniani.

Naye Katibu Mkuu wa CPA Dk. Shija aliupongeza uwamuzi wa Viongozi na wananchi wa Zanzibar kwa kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imeonyesha mfano wa kuleta utulivu na amani na kuwa mfano mzuri wa kusaidia utatuzi wa migogoro katika nchi za Jumuiya ya Madola.

Halikadhalika alisema katika kuadhimisha miaka 100 ya Jumuiya ya Madola, Jumuiya hiyo imekusudia kufanya mabadiliko ya kuimarisha Demokrasia kwa lengo la kuandaa mazingira mazuri kwa vizazi vijavyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.