Habari za Punde

MAJADILIANO KUFUFUA MIFUKO YA AK, JK

Na Ali Mohamed, Maelezo

Mifuko ya mikopo ya JK na AK inatarajiwa kuanza kutolewa tena kwa wananchi baada baada ya majadiliano kati ya Wizara inayoshughulikia mikopo hiyo, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na Beki Kuu (BoT).

Akifungua semina ya siku moja ya kutathmini mifuko hiyo katika hoteli ya Bwawani Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Haroun Ali Suleiman alisema Wizara inafanya tathmini ya kina juu ya namna ya kutoa mikopo hiyo kwa wananchi.

Alisema mikopo hiyo ilikumbwa na changamoto nyingi za uendeshaji na marejesho hali iliyopelekea kutofikiwa lengo la mikopo hiyo la kupunguza umasikini kwa wananchi wa kawaida.

Aidha aliwataka wajumbe wa tathmini hiyo ambao ni maafisa wa mikopo, Waratibu, masheha, Maafisa tawala na wataalamu mbali mbali kutathmini kwa makini na kuja na njia muafaka itakayoiwezesha Wizara kumudu kuendesha mifuko hiyo na kufikia malengo.

Waziri Haroun alisisitiza kuwa elimu itapewa kipaumbele na suala la kurejeshwa mikopo kwa awamu hiyo ni la lazima na wala makosa yaliyofanyika hayawezi kurejewa tena.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Asha Adulla Ali alisema awamu hiyo inayotarajiwa kuanza baada ya majadiliano hayo kuwajibika kwa kila mtu na kurejeshwa mikopo yatakuwa ni masual ya lazima.

Alisema serikali ya awamu ya saba ina nia ya thati ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ndio maana ya kuundwa kwa Wizara ya uwezeshaji hivyo hakutokuwepo na muhali wa aina yoyote kwa mtu yoyote.

Mkurugenzi wa masoko wa PBZ Said Mohamed Said alisema fedha nyingi za mikopo hiyo hazijarejeshwa na baadhi ya mikopo hiyo muda wake wa kurejeshwa umekwisha.

Alizitaja baadhi ya sababu za kushindwa kwa wakopaji kurejesha fedha hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa elimu kabla ya kutolewa kwa mikopo na hali ngumu ya maisha ambayo inawalazimisha wananchi kutumia fedha za mkopo kwa mahitaji ya maisha badala kuzalisha.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mikopo Bihindi Nassor Khatib alizitaja sababu nyengine za kutorejeshwa mikopo hiyo kuwa ni kuwepo kwa dhana baadhi ya wananchi kuwa mikopo hiyo ni zawadi za Marais baada ya kuwapia kura.

Alisema dhana hiyo pamoja na dhana ya kuwa mikopo ya serikali ni sadaka na ujanja wa baadhi ya wananchi zimekuwa ni vikwazo kwa marejesho ya mikopo hiyo ambapo imekuwa ikitumiwa kinyume na malengo.

Nao washiriki wa semina hiyo walielekeza lawama kwa PBZ kwa kuonesha udhaifu katika kufuatilia mikopo hiyo na baadhi ya masheha kuidhinisha majina ya watu ambao walikuwa hawana uwezo wa kukopa na kurejesha.

Walishauri kupitiwa upya kwa miundo ya mikopo hiyo sambamba na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza kwa kuweka sheria na mikakakti itakayohakikisha fedha hizo zinarejeshwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.