Habari za Punde

MAJI TAKA NA AFYA ZA WATOTO






Leo hii katika eneo la majumba ya Michenzani (Jumba na 3) nimeshuhudia watoto wadogo wakicheza katika mazingira hatari kwa afya zao. Nimeshuhudia majitaka yakichirizika na kutuwama katika sehemu mbalimbali za maeneo wanayocheza watoto.

Maelezo ambayo nimeyapata kutoka kwa watoto hao, baadhi ya watoto wenzao huyanywa maji hayo kama sehemu ya kupoza kiu zao wakati wakiwa katika harakati za kucheza. Kusema kweli kwa mujibu wa utafiti wangu wa haraka haraka hakuna jitihada yeyote yakunusuru watoto hao kutoka katika mazingira hatarishi aidha hakuna uangalizi wowote wa karibu kwa watoto hao kutoka kwa wazazi au walezi wao. Ninaamini huenda katika eneo hili tayari watoto wanaathirika na uchafuzi huu wa mazingira.

My concern ni kwamba serikali imekuwa na mikakati mingi ya utekelezaji wa sera na majukumu yake kwenye maeneo ya afya na utunzaji wa mazingira na kinga dhidi ya magonjwa ya milipuko. Halikadhalika, serikali imekuwa na watumishi wanaosimamia maeneo hayo ambao wanalipwa mishahara kwa kazi hizo.

 Vilevile, katika maeneo ya wananchi kunawawakilishi wa wananchi wakiwemo wabunge, wawakilishi, madiwani, masheha, etc, lakini kwa jinsi tatizo lilivyosugu inakuwa vigumu kuaminni kuwa kati ya wahusika wote hao hakuna hata mmoja wao ambaye hajawahi kuona tatizo hili?

Hivi karibuni Mh Rais Dkt Ali Mohammed Shein alisisitiza juu ya usafi wa mazingira na kuweka maeneo yetu safi. Ni wazi kuwa juhudi za wananchi kama hazitaungwa mkono na wahusika katika ngazi mbalimbali ni wazi kuwa hata maagizo ya Mh Rais hayasimamiwi kikamilifu na wale ambao amewapa maagizo husika.

Kwa mfano, tatizo la kuchirizika kwa majitaka ambayo watoto wanayanywa linahitaji nguvu ya serikali au mamlaka husika kuweza kuchimba makaro mapya au kukarabati yaliyokuwepo kuepusha kadhia ya magonjwa ya milipuko. Sitaona ajabu siku kipindupindu kikizuka katika maeneo hayo serikali na watendaji wake wote watahamia kwenye aneo la tukio na kutumia rasilimali nyingi badala ya kuweka mazingira mazuri kwa wakati huu kwa kutumia rasilimali kidogo. 

Mwisho, niwakumbushe wananchi wenzangu kuwa wajibu wa kwanza kuhakikisha kuwa mazingira yetu yanakuwa safi ni kwa wananchi wenyewe kujihusisha katika kuyasimamia mazingira yao na kuishirikisha serikali na wawakillishi wake katika kupata suluhu ya matatizo yaliyokuwepo.

Mwisho ninakushukuru sana Bw. Othman kwa kuwa na platform hii ambayo nina hakika inasaidia katika kufikisha matatizo na mafanikio yaliyopo katika jamii zetu.

Shukran Mdau kwa taarifa. Tupo katika kuwajibika na kama mtu yeyote ana picha, habari, taarifa za kuendeleza, kuelimisha, kurekebisha zote tunazipokea na tutaziweka almuradi zisiwe za kuchafua hali ya hewa tu. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.