Habari za Punde

SERIKALI KUSAIDIA WAGONJWA WA KISUKARI - DK SHEIN

Na Rajab Mkasaba, Ikulu


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk Ali Mohamed Shein,akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Jumuiya ya watu Wanaoishi na maradhi ya kisukari Zanzibar,waliopofika Ikulu Mjini Zanzibar,kumpongeza Rais,na kufanya mazungumzo na jumuiya hiyo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ameuhakikishia uongozi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na maradhi ya Kisukari Zanzibar kuwa serikali itaongeza huduma kwa wagonjwa wa kisukari na kwa kupitia Wizara ya Afya italisimamia suala la ujenzi wa kliniki yao.

Rais  Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar wakati walipokuwa na mazungumzo na uongozi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Kisukari Zanzibar, ujumbe huo ulifika kwa ajili ya mazungumzo sambamba na kumpongeza Rais kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Katika maelezo yake, Dk. Shein aliwapa pole wale wote wanaokabiliwa na ungonjwa huo na kueleza kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha huduma wanazopewa  zinaimarishwa zaidi ikiwa ni pamoja na kuongeza madaktari watakao washughulikia wagonjwa hao.

Mbali na huduma hizo Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya italisimamia suala la ujenzi wa Kliniki ya wagonjwa wa kisukari wazo ambalo lilianzwa kutolewa na Rais Mstafu Dk. Amani Abeid Karume.

Dk. Shein alisema kuwa kujengwa kwa kituo hicho kutasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa elimu, tiba, kinga pamoja na mambo mengine muhimu ya kuasaidia wagonjwa wa kisukari hapa Zanzibar.

Alisema kuwa juhudi  zitachukuliwa katika kuhakikisha eneo zuri linapatikana kwa ajili ya ujenzi wa kliniki hiyo na kuhakikisha kuwa ndani ya miaka mitano hatua kubwa inafikiwa na kusisitiza haja ya kuwepo kituo cha utafiti juu ya maradhi hayo katika kliniki hiyo.

Aidha, Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Jumuiya hiyo kwa kuendeleza vyema Jumuiya hiyo na kueleza haja ya kuandaa timu ya madaktari wataalamu watakaotoa huduma kwa wagonjwa wa kisukari Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa kutokana na wagonjwa wa maradhi hayo kuongezeka siku hadi siku inapelekea madaktari wanaotoa huduma kwa wagonjwa hao kuwa haba na kutoa pongezi kwa madaktari bingwa wanaotoa huduma hivi sasa juu ya maradhi hayo hapa Zanzibar.

Pia, Dk. Shein alisisitiza haja ya kushajihishwa wananchi kufanya mazoezi, pamoja na kuwaelimisha wale wote waliokuwa hawajapata maradhi hayo ili waweze kujikinga.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Bwana Waziri Said Othman alimueleza Dk. Shein kuwa kuwepo kwa kliniki hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma kwa wagonjwa hao pamoja na kusisitiza haja ya kufanyiwa utafiti kwa dawa za kienyeji ambazo zinaweza nazo kusaidia katka kutoa tiba ya maradhi hayo.

Mapema Katibu wa Jumuiya hiyo, Ali Zubeir Juma alisema kuwa azma ya kujenga kliniki ya watu wanaoishi na kisukari ipo hasa ikizingatiwa kuwa uongezeko la wagonjwa hao linakuwa kwa kasi hapa Zanzibar.

Alisema kuwa inakisiwa kuwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara zina watu milioni 19 wanaosumbuliwa na maradhi ya kisukari ambapo kwa upande wa hapa Zanzibar kuna watu zaidi ya elfu sita katika kipindi cha kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka jana 2010.

Aidha, alisema kuwa kama ilivyo kwa nchi nyengine za Kiafrika pia, wagonjwa wa kisukari waliopo hapa Zanzibar wamekuwa wakichelewa kugundulikana na maradhi, kuchelewa kupata matibabu, upungufu wa madaktari na taaluma chache yamaradhi hayo.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo imepelekea nafasi iliyopo ambayo hutolewa huduma kwa wagonjwa wa kisukari katika hospitali ya MnaziMmoja ni ndogo na haitoshi kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa.

Nae Dk. Faiza Kassim Suleiman alimueleza Dk. Shein kuwa juhudi zinazochukuliwa ni kubwa sana katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa kisukari ambapo tayari kuna vituo vinane, Pemba vitano na Unguja vitatu na kusisitiza kuwa mkazo mkubwa uliopo hivi sasa ni kutoa elimu na kushajihisha ili kuepuka wananchi wasipate maradhi hayo.

Alisema kuwa kwa upande wa kituo cha hospitali ya MnaziMmoja peke yake kina wagonjwa 4000 na kueleza kwa umefika wakati kwa wananchi kubadilika ikiwa ni pamoja na kuwa na uangalifu wa vyakula wanavyokula, kufanya mazoezi na kujiepusha na kutumia vileo vya aina zote.

Sambamba na hayo, Dk. Faiza alisisitiza haja ya viongozi wakiwemo Wawakilishi, kulizungumzia kwa upeo mkubwa zaidi suala la maradhi ya kisukari kwa wananchi katika shughuli zao zote kama linavyozungumzwa suala la maambuziki ya ukimwi hivi sasa, hiyo ni kutokana na ugonjwa huo kushika kasi hapa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.