Alikwama 'Dar Airport' kwa kutokuwa na visa ya Marekani
Na Ameir Khalid
MSANII maarufu wa mashairi na mwandishi wa vitabu mzee Haji Gora Haji, ameelezea kusikitishwa kwake na kitendo cha kukwamishwa kusafiri kwenda nchini Colombia ambako alialikwa kuhudhuria tamasha la utamaduni na uandishi.
Akizungumza na Zanzibar Leo jana, Gora alisema safari hiyo iliyokuwa imeratibiwa kupitia taasisi ya Tamasha la Filamu za Nchi za Majahazi (ZIFF), haikuweza kufanyika baada ya kufika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kukuta akiwekewa kizingiti.
Mkongwe huyo wa sanaa ya mashairi, alitakiwa kuondoka nchini Juni 30, 2011 kwa ajili ya tamasha hilo lililokuwa limepangwa kuanza Julai 2 hadi 9, mwaka huu, ambapo alifika uwanja wa ndege Dar es Salaam kwa ajili ya kupanda ndege ya kumchukua hadi Dubai (UAE).
Alifafanua kuwa safari yake kwenda Dubai ilipaswa kuanza saa 10:00 alasiri na kwamba baadae angebadilisha ndege Dubai kupitia Marekani kabla kuhitimisha safari hiyo nchini Colombia.
Hata hivyo, alidai alipokuwa Dar es Salaam alitakiwa kuonesha visa ya Marekani, ambayo alielezwa kuwa ni lazima hata kama anapitia huko kwa kubadilisha ndege ya nchi nyengine.
"'Jambo la kushangaza maofisa wa uwanja wa ndege Dar es Salaam waliniambia kuwa, lazima niwe na viza ya Marekani ndipo niruhusiwe kutua nchi hiyo kwa ajili ya kubadilisha ndege'', alifafanua.
Baada ya kuelezwa hivyo, Gora alisema jitihada za kupata visa hiyo zilifanikiwa baada ya wiki moja, lakini hakuweza kusafiri kwa vile alikuwa ameshachelewa.
Mzee Gora alihoji iwapo sheria hiyo iko katika nchi zote au ni Marekani pekee.
Hata hivyo Zanzibar Leo ilifanikiwa kumpata mtu aliyeratibu safari hiyo Farida Said ambaye alieleza kuwa, visa ya Colombia ilipatikana miezi miwili kabla safari, lakini hakuwa anafahamu taaribu mpya za ubalozi wa Marekani.
Aidha alisema hawakuona sababu ya kupata visa ya Marekani kwa kuwa Gora hakutarajiwa kutoka nje ya uwanja bali alikuwa asubiri ndege nyengine.
Akifafanua zaidi, Farida alidai kuwa ubalozi wa Marekani uliwaambia kwamba taarifa za mabadiliko hayo zilitolewa zamani katika nchi zote, kwamba hata mtu awe anabakia uwanjani ni lazima apate visa ya nchi hiyo.
"Tulimpa mtu wa kumshughulikia uwanjani, tulipopata taarifa kuwa amekwama, tulimfuata na ilibidi alale hoteli, na baadae tukaanza taratibu za kutafuta visa, lakini ikachuka muda kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuingiliana na siku ya uhuru wa Marekani pamoja na Saba Saba", alifafanua.
Alisema hata pale walipofanikiwa kuipata, Julai 7, ingekuwa vigumu kwake kusafiri kwani tamasha hilo lilikuwa linamalizika Julai 9, na walielezwa kuwa asingeweza kusoma mashairi.
Pamoja na usumbufu huo, Farida alieleza kuwa kwa vile mzee Gora amepata visa ya mwaka mzima, huenda akafikiriwa kupatiwa mualiko kwa tamasha la mwakani
No comments:
Post a Comment