Habari za Punde

DKT BILAL AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA 31 WA WAKUU WA NCHI ZA SADC NCHINI ANGOLA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amemwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) katika mkutano wake mkuu wa 31 ambao ulihusisha pia uchaguzi wa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa mwaka 2011/12, ambapo Rais Jose Eduardo Dos Santos wa Angola amekabidhiwa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya hiyo kutoka kwa Rais wa Namibia Hifikepunye Pohamba.


Akipokea nafasi hiyo, Rais Dos Santos alifafanua nia ya SADC kuendelea kushikamana na kudumisha amani katika nchi wanachama, huku akieleza kuwa suala la ukosefu wa ajira kwa wananchi wa nchi hizi hasa vijana linapaswa kutazamwa kwa jicho la karibu kwa kuwa ni sawa na bomu linaloweza kulipuka wakati wowote kama halitapatiwa ufumbuzi.

Katika mkutano huo mambo kadhaa yalijadiliwa na mengi yaliakisi hali ya amani na utulivu katika nchi wanachama na kubwa likawa kwa nchi hizi kukubaliana kwa kauli moja kutoa msaada wa hali na mali kwa nchi ya Somalia inayokabiliwa na baa la njaa. Nchi ya Afrika Kusini ilikubali kutoa usafiri wa michango yote itakayotakiwa kwenda Somalia wakati Tanzania ilitangaza kuhusu mchango wake ambao alikwishaahidiwa Rais wa Somalia Abdullah Yusuf Ahmed alipokuja kumtembelea Rais Jakaya Kikwete na kuomba msaada wa hali na mali kwa nchi yake, jambo ambalo lilikubaliwa kwa uharaka na Tanzania.

Mkutano huo licha ya kujadili suala la hali ya kisiasa nchini Zimbabwe na Madagascar, pia ulikamilika kwa kutiliana saini ya makubaliano katika mikataba mitatu baina ya nchi wanachama iliyohusu mashirikiano katika kudhibiti fedha chafu, Kupitishwa kwa katiba ya mashirikiano kwa majeshi ya Polisi katika nchi wanachama, sambamba na ule wa utunzaji wa mazingira katika ukanda wa Kavango na Zambezi.

Mkutano huo ulimchagua Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kuwa Mwenyekiti wa Kamati nyeti ya Siasa, Ulinzi na Usalama huku Makamu Mwenyekiti wake akichaguliwa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania. Nafasi ya Mwenyekiti itabakia kwa mwenyeji wa mkutano huo Angola hadi mkutano mkuu mwingine utakapofanyika mwakani nchini Msumbiji na hivyo nchi hiyo kupewa jukumu hilo kwa mwaka 2012/13.

Katika mkutano huu nafasi ya Tanzania imebakia kuonekana kuwa ya kuigwa kutokana na kuwa na hali tulivu sambamba na kuwa eneo la kuigwa kulinganisha na mataifa mengine.

Katika mkutano huo; Makamu wa Rais aliambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo ambaye alitangulia Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Ulinzi ambaye pia alitangulia, Hussein Mwinyi na Waziri wa Viwanda na Biashara Cyril Chami.

Imetolewa na: Boniphace Makene
Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ijumaa Agosti 19, 2011

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.