Habari za Punde

KONGAMANO KUBWA CENTRAL LAJA

Litajadili kuporomoka soka la vijana, kulifufua

Na Ali Cheupe, ZJMMC

KAMATI ya Central Taifa Zanzibar, inakusudia kuandaa kongamano maalumu litakalojumuisha viongozi, wadau na wanasoka wa zamani waliopitia katika ngazi hizo ili kukusanya mawazo ya jinsi ya kuboresha ligi zake.


Wazo hilo limekuja kutokana na hali ya kudumaa kwa soka la vijana, huku migogoro kadhaa ikizikumba klabu sambamba na viongozi wanaoshughulikia ligi hizo.

Katibu wa kamati hiyo Abdallah Thabit ‘Dula Sunday’, amesema kongamano hilo limepangwa kufanyika Agosti 28, mwaka huu katika ukumbi wa juu hoteli ya Bwawani, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdillah Jihad Hassan.

Thabiti alisema ana matumaini makubwa kuwa, mkusanyiko huo wa wachezaji hao wakongwe, utakuja na fikra mpya za kuendeleza soka la vijana na kurejesha hadhi ya ligi za madaraja hayo.

“Naamini kupitia kongamano hilo tutapata mawazo, changamoto, ushauri na hata ubunifu kutoka kwa wadau ili kuboresha na kurejesha hadhi ya soka la vijana hapa Zanzibar”, alisema Thabit.

Aliwataja baadhi ya wachezaji walioalikwa katika kongamano hilo ambao walipitia soka la vijana kuwa ni pamoja na Ali Sharif 'Adolph', Hashim Salum, Salum Bausi, Abdallah Maulid, Zahor Salum, Abdulwakati Juma na Ali Bushiri.

Kwa upande wake, Ali Sharif 'Adolph', alipongeza uamuzi wa kuwakutanisha wanasoka hao akiamini mchango wao utaweza kuleta mafanikio makubwa endapo viongozi na wachezaji wataufuata.

Adolph aliyekuwa miongoni mwa wanasoka walioiletea sifa kubwa klabu kongwe ya Malindi, alizitaja changamoto zinazozikabili ligi za vijana kwa sasa, kuwa ni pamoja uchakavu wa viwanja vya Mnazimmoja vilivyoibua wachezaji wengi vijana waliokuja kutamba katika timu kubwa na zile za taifa.

Alitoa wito kwa serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuangalia uwezekano wa kuvitengeneza upya viwanja hivyo ikiwa pamoja na kurekebisha miundombinu ili maji yasiweze kutuwama na hivyo kuwanyima vijana fursa ya kujiendeleza kimichezo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.