Mengi aliyofunza Kuleta ulimwenguni
Masudi unauliza Dhiki yetu kitu gani
Maji yakiadimika Viumbe tuko tabuni
Maji ni zawadi kubwa Kaileta Rahmani
Huwezi kukaa kucha Usi yatie mwilini
Tuombe kutwa na kucha Yaweko ulimwenguni
Maji yakiadimika Viumbe tuko tabuni
Si kwa mtu peke yake Bali hata hayawani
Akila majani yake Na maji yawe usoni
Lazima uyakumbuke Au mnyama haponi
Maji yakiadimika Viumbe tuko tabuni
Chakula hutokipika Sheti kwa maji yakini
Au la kunadhifika Ndipo uweke jikoni
Chungu hakitochemka Kikikosa maji ndani
Maji yakiadimika Viumbe tuko tabuni
Kisha unapoamka Uso uko ghadhabuni
Tena umetatanika Hata macho huyaoni
Maji ukishampaka Mara huwa furahani
Maji yakiadimika Viumbe tuko tabuni
Nguo ikisha chafuka Huwezitia mwilini
Haiwezi kufulika Japo uwe na sabuni
Lazima maji kufika Ndio utie chanoni
Maji yakiadimika Viumbe tuko tabuni
Chai haijapikika Kwa sukari na majani
Sheti maji kuchemka Yawemo sufuriani
Ndipo utapotosheka Ukaitia bulini
Maji yakiadimika Viumbe tuko tabuni
Nyumba zisinge jengeka Hili lifikirieni
Mvua ikitoweka Roho zetu zina beni
Vyakula kuharibika Viliomo mashambani
Maji yakiadimika Viumbe tuko tabuni
Beti tisa nimefika Kalamu naweka chini
Na mabingwa wasifika Na mate yapo kinywani
Na basi nna haraka Nakimbilia jikoni
Maji yakiadimika Viumbe tuko tabuni
No comments:
Post a Comment