Habari za Punde

VYMA VITATU VYA MICHEZO VYAANZA MBIO ZA UCHAGUZI

BTMZ yataka watakaojitokeza kuelewa tafsiri za sheria

Na Salum Vuai, Maelezo

BAADA ya kupita muda mrefu bila kufanya chaguzi, vyama vitatu vya michezo Zanzibar vimeanza mchakato wa kuingia katika hatua hiyo ya kidemokrasia.



Kwa mujibu wa taarifa za Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) Hassan Tawakal Khairallah, vyama hivyo ni kile cha riadha (ZAAA), mpira wa kikapu (BAZA) na Chama cha Netiboli (CHANEZA).

Khairallah amesema, jana baraza lake lilikuwa na kikao na makatibu wa vyama hivyo, ambapo mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na kuandaa uchaguzi utakaokuwa mzuri na wa haki kwa lengo la kuendeleza michezo nchini.

Alifahamisha kuwa kimsingi viongozi wa vyama hivyo wameonesha dhamira na hamu ya kutaka kufanya chaguzi zao, na kwamba walieleza wazi haja kwa wadau mbalimbali kujitokeza kugombea wakati utakapofika.

Ili kuelekea uchaguzi mkuu, Katibu huyo alisema chama cha ZAAA kitafanya mkutano na wanachama wake Septemba 3, na ZAAA itafanya hivyoi Septemba 4, ili kwa pamoja kupitia rasimu za katiba zao, na kuhakikisha kasoro zozote zilizomo zinarekebishwa, kabla kuziwasilisha barazani ili zibarikiwe na kuwa katiba.

Hata hivyo, alieleza kuwa CHANEZA imepewa muda wa kuifanyia marekebisho rasimu yake baada ya kuonekana ina mapungufu mengi, na baadae itaangalia hatua nyengine.

"Tumekubaliana kufanya marekebisho ikiwa pamoja na vyama kukaa na wenzao kwa sababu tunalenga kufanya chaguzi zilizo bora, ili kuondoa migogoro na kuleta maendeleo ya michezo",alifafanua.

Aidha alifahamisha kuwa kila chama kinatakiwa kuwa na kamati tafauti ikiwemo ya uchaguzi na rufaa, ambazo zinatarajiwa kufanya vyama hivyo kuongozwa kwa misingi ya demokrasia na uwazi.

Katibu huyo alisisitiza kuwa vyama vyote ni lazima viwe na sura ya kitaifa na vising'ang'anie kufanya kazi mijini pekee.

Alitoa wito kwa wadau na wanamichezo wote watakaotaka kugombea nafasi za uingozi, kuhakikisha wana uelewa wa kutosha wa nafasi wanazotaka kuwania, ili wakichaguliwa kusijitokeze makosa ya kushindwa kutafsiri sheria.

Chaguzi zote hizo zitagharamiwa na BTMZ ikiwa pamoja na nauli za wajumbe wa Pemba, posho na mahitaji mengine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.