Na Mwantanga Ame
UMOJA wa wake wa Viongozi wamesema msiba uliotokea wa kupoteza maisha ya wananchi wakiwemo wanawake na watoto katika meli ya Mv. Spice Islander umeigusa taasisi hiyo.
Mwenyekiti wa Umoja huo Mke wa Makamu wa Pili wa Rais Mama Asha Seif Iddi, aliyasema hayo jana baada ya kupokea msaada wa shilingi milioni 10 kutoka kwa Mwenyekiti wa kampuni ya Usafirishaji na upakuzi wa mizigo katika kiwanja cha Ndege cha Zanzibar, Mohammed Raza.
Mama Asha alisema vifo vilivyotokea hasa vya wanawake na watoto vimeugusa kwa kiasi kikubwa umoja huo na watahakikisha kuwa wanashirikiana na jamii katika msiba huo.
Alisema kutokea kwa maafa hayo kwa kiasi kikubwa kutaweza kuwaathiri wanawake wengi kutokana na baadhi yao kupotelewa na waume wao huku huku baadhi ya wazazi wao kufariki wote na kuacha kundi la watoto yatima.
Alisema jami itapaswa kuona inazipa msaada familia hizo kwa hivi sasa zipo katika wakati mgumu wa kujiendesha maisha yao kutokana na kukosa wazazi wote wawili.
Mapema Mwenyeki wa Kampuni hiyo, Mohammed Raza alieleza juu ya kusikitishwa na tukio hilo na kuiuomba umoja huo kuona inawafikia vilivyo waathirika wa tukio hilo na kuwapa misaada.
Alisema kuwepo kwa tukio hilo hivi sasa sehemu kubwa ya jamii ilikumbwa na matatizo hayo itakuwa inahitaji kupata misaada kwa vile kutakuwa na mayatima wengi.
Alisema kampuni yao itakuwa tayari kuona inashirikiana na umoja huo kila pale inapobidi kwa vile imeonekana kupenda kuleta maendeleo katika nchi hasa yale yanayowahusu wanawake na watoto.
Katika hatua nyengine, KANISA Anglikana Zanzibar litaendesha sala maalum ya kuwaombea marehemu na waathirika wa ajali ya kuzama meli ya Mv Spice Islander.
Viongozi wa kanisa hilo, walieleza hayo wakati wakikabidhi mchango wa shilingi 500,000 kwa Mwenyekiti wa Kamati ya maafa, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, ikiwa ni mchango wa kanisa hilo kwa waathirika hao.
Kasisi kiongozi wa kanisa la Anglikana Zanzibar Michael Hafidh, alisema waumini wa kanisa hilo wameguswa na msiba huo, hivyo mbali ya kutoa mchango huo pia watafanya sala maalum ya kuwaombea marehemu na waathirika.
Mchungaji huyo alisema waumini wa kanisa hilo wako pamoja na wafiwa na waliojeruhiwa kutokana na ajali hiyo na watakuwa tayari kuona wanaandaa sala maalum wiki hii kwa ajili ya kuwakumbuka waathirika wa tukio hilo.
Alisema sehemu kubwa ya jamii iliwategemea sana wananchi hao katika shughuli mbali mbali za kiuchumi na ukuwaji wa maendeleo lakini jambo la kusikitisha kuona nguvu kazi hiyo imeondoka duniani kutokana na ajali hiyo.
Mchungaji Hafidh alizitaka familia zilizoondokewa na watu kuwa na moyo wa subira kwani Mungu amewapenda na wawe wenye kusubiri pale wanapopatwa na misiba mizito ikiwemo ya aina hiyo.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, alisema serikali imefarajika kuona wananchi wote wamekuwa wamoja kushiriki katika msiba huo bila ya kujali irtikadi za kidini.
CHANZO: Zanzibar Leo
No comments:
Post a Comment