RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dr. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa mabadiliko katika sekta ya afya ni hatua muhimu ambayo inaweza kufikiwa iwapo kila mtumishi katika sekta hiyo atatekeleza wajibu wake ipasavyo.
Dk. Shein alieleza hayo leo huko katika ukumbi wa Misali Sun Set Beach Hotel, iliyopo Wesha Pemba, katika ufunguzi wa Mkutano mkuu wa sita wenye lengo la kuwaunganisha watendaji wote wakuu wa sekta ya afya pamoja na kutathmini shughuli zao.
Katika hotuba yake Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake na kauli mbiu yamwaka huu ya mkutano huo inayosema “Lazima tubadilike katika kutoa huduma bora za afya” na kushauri kauli mbiu hiyo itumiwe na kila mtendaji katika Wizara hiyo.
“Maisha ya jana si sawa na ya leo”,alisisitiza Dk. Shein na kueleza kuwa suala la kubadilika lina umuhimu mkubwa katika nchi yenye maendeleo “Mabadiliko hayaepukiki katika nchi yenye maendeleo” aliendelea kueleza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alipongeza wazo la kushirikisha wadau mbali mbali wa ndani na nje ya Zanzibar kwa nia ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta ya afya hapa nchini.
Alieleza matumaini yake ya kufanikiwa kwa mkutano huo wa siku mbili kwa kuzingatia mada zinazozungumzwa na fursa za majadiliano watakayoyapata wajumbe.
Alisema kuwa wajumbe wana fursa ya kuzungumzia tafiti na fursa za masomo zilizopo katika sekta ya afya ambapo yote hayo yatasaidia katika kukabiliana na changamoto ziliopo katika sekta ya afya.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwakaribisha wageni waliotoka nje ya Zanzibar na kueleza kuridhishwa na maandalizi ya mkutano huo uliofanyika kwa mara ya kwanza kisiwani Pemba.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alibainisha malengo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuelekea 2015 yanayozingatia Malengo ya Milenia katika sekta ya afya.
Alieleza dhima muhimuiliyonayo Wizara ya Afya ya kuhakikisha kufikiwa wka Malengo ya Milenia sambamba na kutekeleza Malengo ya Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini MKUZA 11 na Dira ya 2020.
Alibainisha kuridhishwa kwakwe na utendaji wa Wizara ya Afya na kueleza kuwa yeye binafsi ameridhishwa na mafanikio yaliopatikana katika mradi wa kupambana na Malaria wenye kauli mbiu “MALIZA MALARIA ZANZIBAR”, na kufikia chini ya silimia 1.
Aidha, alisifu mafanikio katika kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi ambapo pamoja na mafanikio hayo, aliitaka Wizara iengeze jitihada maradufu. Pia aliipongeza Wizara hiyo kwa kuwa ya mwanzo kuweka mfuko wa kuchangia huduma za afya ambao utasaidia bajeti ya serikali.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani zake kutokana na mchango wa washirika wa maendeleo na wadau wengine wanaoisaidia Zanzibar hasa katika sekta ya afya na kueleza kuwa mchango wao umeweza kusaidia kufikia malengo ya Wizara hiyo.
Nae Waziri wa Afya Mhe. Juma Duni Haji, alieleza mafanikio yaliopatikana katika sekta ya afya sanjari na mikakati ya kuimarisha sekta hiyo iliyowekwa.
Mapema Dk. Shein alitembelea mabanda mbali mbali ya maonesho katika eneo hilo la Hoteli ya Misali yalitengezwa maalum kwa lengo la kuonesha mambo mambali mbali yanahusiana na huduma huduma ya afya.
No comments:
Post a Comment