Habari za Punde

DK SHEIN MGENI RASMI SIKU YA UKIMWI

Na Is`haka Mohammed, Pemba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasimi katika kilele cha maadhimisho siku ya UKIMWI duniani kitaifa huko Makombeni wilaya ya Mkoani.

Akizungumza na gazeti hili, Mratibu wa Tume ya UKIMWI Pemba, Nassor Ali Abdalla huko Ofisini kwake Chake Chake, alisema matayarisho ya shughuli hiyo yanaendelea vizuri hadi sasa.


Alisema katika maadhimisho ya mwaka huu kumepangwa kufanyika shughuli mbalimbali, yakiwemo maonyesho yatayoonyesha kazi na huduma zinazotolewa na Taasisi zinazopambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI visiwani Zanzibar.

Alisema licha ya maonesho hayo na hotuba ya mgeni rasmi pia kutakuwepo burudani tofauti kama vile tenzi ngoma, nyimbo na ngoma na michezo ya kuigiza kutoka kwa wasanii wa ngoma za asili na za kisasa ambazo zitatoa ujumbe kuhusiana na hali ya maambukizi ya UKIMWI na unyanyapaa Zanzibar.

Mratibu huyo alisema kuwa siku hiyo kutakuwa na uzinduzi wa tovuti ya Tume ya UKIMWI Zanzibar, ambayo itatoa fursa kwa wananchi mbali kupata taarifa za UKIMWI kupitia tovuti hiyo.

Nassor alisema licha ya mambo hayo yatakayofanyika siku ya Disemba mosi ambayo ndiyo siku ya kilele, pia maadhimisho hayo yataadhimishwa kila wilaya kwa kufanya makongamano mbalimbali yatakayojadili suala la ukimwi Zanzibar.

Kwa upande mwengine Nassor aliwataka wananchi wa kisiwa cha Pemba kufika kwa wingi katika siku hiyo ya kilele, na kwenda kusikiliza kauli ya serikali juu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi visiwani humo.

Pia alisema kuhudhuria kwao huko kutawapa nafasi ya kujua mengi kuhusiana na hali ya ukimwi na VVU visiwani Zanzibar kupitia maonyesho na burudani mbali mbali zitakavyokuwepo na kutoa ujumkbe mahsusi.

Maadhimisho ya ukimwi huadhimishwa kila ifikapo Disemba mosi kila mwaka, na kwa mwaka huu Zanzibar itaadhimishwa kitaifa huko Makombeni Wilaya ya Mkoani na Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohammed Shein.

Maadhimisho ya mwaka uliopita yalifanyika Bwawani mjini Unguja na Mgeni Rasmi alikuwa ni Makamo wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.