Habari za Punde

KOCHA MWENGINE AITOSA ZANZIBAR HEROES


KOCHA Msaidizi wa timu ya taifa ya soka ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' Abdelfatah Abass akiwa bandarini Dar es Salaam jana kwenda Zanzibar baada ya kuamua kukiacha kikosi cha timu hiyo kilichopo katika michuano ya 'Tusker Challenge Cup' yanayofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.( Picha na Haroub Hussein).

Ni Abdelfatah Abbas aliyekimbia kuingiliwa kazi

Na Salum Vuai, Dar es Salaam

KATIKA hali inayoonesha mambo hayaendi vizuri ndani ya kambi ya timu ya taifa ya soka Zanzíbar ‘The Zanzíbar Heroes’, msaidizi Kocha Mkuu wa timu hiyo Abdelfatah Abbas, ameondoka na kurejea Zanzíbar.

Mwandishi wa habarí hizi, alibahatika kumuona Mmisri huyo akipanda boti ya Kilimanjaro iliyoondoka saa 3:30 jana asubuhi katika bandari ya Dar es Salaam.

Alipoulizwa sababu ya kuondoka kwake, Abbas alidai kuwa, hawezi kukubali kuingiliwa katika kazi yake hiyo na baadhi ya viongozi wa Chama cha Soka Zanzíbar (ZFA) walioambatana na kikosi hicho kwenye michuano ya Chalenji inayoendelea jijini hapa.

Alifahamisha kuwa, katika mchezo wa pili dhidi ya Burundi ambapo timu hizo zilishindwa kufungana, wakati wa mapumziko, viongozi hao walimsikitisha kwa kutaka kumzuia asifanye kazi yake kama taaluma yake inavyomuelekeza.


“Mimi si kocha wa kuokota, nimefanya kazi hii miaka 27 na timu mbalimbali zilizo kubwa, ninapoamua kubadilisha mchezaji, au mfumo wa kucheza huwa nina malengo yangu ambayo ni manufaa kwa timu, inakuwaje nibanwe na kuzuiwa kusema na wachezaji, je likitota si nitaambiwa nimeshindwa kazi?” alilalamika kocha huyo.

Aidha, alisema uamuzi wa kuiacha solemba timu hiyo, unalenga kulinda ‘proffession’ yake, hivyo ni vyema akae pembeni, ingawa anatamani timu hiyo ishinde mchezo wake dhidi ya Somalia na kutinga robo fainali ya mashindano hayo hadi kutwaa ubingwa.

“Baada ya mchezo wa jana (juzi), tukiwa ndani ya basi tunarudi hotelini, niliwaaga wachezaji na kuwaambia wazi kwamba naondoka, huku nikiwatakia mafanikio mbele ya safari”, alieleza Abbas.

Zanzibar Leo ilipowasiliana na mkuu wa msafara wa timu hiyo Mustafa Omar kwa njia ya simu, alionesha mshangao na kusema hana habarí juu ya kuondoka kwa kwamba kocha huyo.

Aidha alidai siku iliyotangulia baada ya mechi ya mwisho na Burundi, hakumbuki kutokea suitafahamu yoyote ndani ya kambi hiyo kuhusiana na kocha huyo.

Naye Kocha Mkuu Hemed Suleiman ‘Moroko’, alisita kueleza kilichojiri na kumtaka mwandishi wetu amuulize Abbas mwenyewe sababu iliyomuondoa.

Kwa upande wake, Rais wa ZFA Ali Ferej Tamim, alisema hana taarifa hiyo, lakini hata hivyo yeye hayuko Dar es Salaam kushughulikia timu bali anahudhuria mashindano hayo kwa nafasi yake katika Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Aidha alisema, Abbas si kocha mkuu wa Zanzíbar Heroes, na kwamba nafasi hiyo imo mikononi mwa Hemed ‘Moroko’.

Abbas anakuwa kocha wa pili kuipa mgongo timu hiyo, kufuatia awali aliyekuwa kocha mkuu Muingereza Stewart John Hall, kuamua kuachia ngazi hivi karibuni.

1 comment:

  1. hizi ni dalili mbaya na zimeanza zamani tangu kambi ya misri kukosekana baadhi ya wachezaji, kukosenaka kocha mkuu, mara kocha mkuu kuachia ngazi na sasa kocha msaidizil. Kiufupi katika mashindano haya hakuna chetu tuwaache wamalize warudi kuendelea na ligi zao za kawaida.Cha muhimu wakae hao viongozi wafahamiane. Masikini naoionea huruma iyo serikali kupoteza hizo hela kuandaa timu . Pole mh Jihadi jitahada zimeoneka ila watendaji wamekuangusha, inabidi ujipange tena.maneno ya wagosi wakaya " timua timua wote"

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.