Habari za Punde

ZANZIBAR NA SHARJAH ZAKUBALIANA KUTAFITI VIANZIO VYA MAJI

Na Rajab Mkasaba, SHARJAH (UAE) 15.11.2011

ZANZIBAR na Sharjah zimekubaliana kuanzisha ushirikiano katika utafiti wa vianzio vya maji vitakavyoihakikishia Zanzibar upatikanaji wa maji safi na salama ya kutosha kwa kwa miaka mingi ijayo.

Makubaliano hayo yalifanyika katika mazungumzo kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Kiongozi wa Sharjah Sheikh Sultan Mohammed Al Qasimi huko mjini Sharjah.


Kiongozi huyo alieleza kuwa Sharja iko tayari kusaidia kufanya utafiti kwa mara nyengine tena katika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya Zanzibar.

Pamoja na mazungumzo hayo, viongozi hao kwa pamoja walieleza haja ya kukuza na kuimaisha uhusiano uliopo kati ya pande mbili hizo.

Katika maelezo yake Dk. Sultan alimueleza Dk. Shein kuwa Sharjah inathamini sana uhusiano uliopo kati yake na Zanzibar na kueleza kuwa Shrajah ina azma ya kufanyia maengenezo makumbusho makubwa ya Zanzibar.

Viongozi hao kwa pamoja pia, waliahidi kushikiana katika kuimaisha sekta za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya elimu, afya, biashara, uwekezaji na nyenginezo.

Dk. Shein alitoa shukurani kwa uwamuzi huo wa Sheikh Sultan wa kusaidia utafiti wa upatikanaji wa maji kwa Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alitembelea afisi za Jumuiya ya Wafayabiashara na Wenyeviwanda wa Sharja na kufanya mazungumzo nao ambapo katika mazungumzo hayo Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla zimepata mafanikio makubwa kutokana na kuwepo kwa amani na Utulivu ambao ndio msingi mkuu wa uwekezaji na biashara na maendeleo kwa jumla.

Alisema kuwa nchi ambayo haina amani na utulivu mara zote haiwezii kuendeleza shughuli zozote za maendeleo zikiwemo za kibiashara na uwekezaji.


Dk. Shein aliwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kuwa kuna uhusiano wa kistoria kati ya Zanzibar na Sharjah na kueleza haja ya kuimarisha uhusiano huo na kuongeza wigo wa kufanyabishara kwa kungiza na kutoa bidhaa.

Adha, aliwashukuru kwa kutoa fursa kwa nchi za nje kufanyabishara na Sharjah.Ambapo pia Dk. Shein aliwaeleza fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar ikiwa ni pamoja na Maeneo Huru ya uwekezaji sanjari na Bandari Huru.

Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa ipo haja kwa pande mbili hizo kuandaa programu za pamoja ambazo zitasaidia katika shughuli za kibiashara na uwekezaji pia, alieleza haja ya kufanya kazi kwa pamoja.

Alieleza kuwa sekta binafsi zikiwajibika ipasavyo zinaweza kuleta mabadiliko ya haraka ya kiuchumi na kueleza kuwa wazo la kuanzisha kituo cha maonyesho ya biashara Zanzibar inapaswa kupewa kipaumbele na kutekelezwa haraka iwezekanavyo.

Dk. Shein alielendelea kusema kuwa kwa vile Sharjah imepiga hatua kubwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Sharjah. Aidha, Dk. Shein alitoa shukurani kwa Sharjah kwa kutoa nafasi za elimu kwa Wazanzibari na kueleza kwamba hatua hiyo itasaidia kuimarisha elimu kwa Zanzibar.

Alieleza kwamba kihistoria Wazanzibari na Sharjah walikuwa wakisafiri kwa majahazi katika safari zao za kibiashara lakini hivi sasa wamekuwa na usafiri wa kuaminika wa ndege na bahari ambao umerahisha safari hizo za kibiashara.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Bwana Ahmed Mohammed AlMidfa, alieleza kuwa hali ya bei ya bidhaa mbali mbali Sharjah ni nafuu ikiliganishwa na maeneo mengine ya Umoja wa Kiarabu, hivyo hali iyo inarahisha shughuli za kibiashara.

Alieleza kuwa Jumuiya hiyo ina mfumo wa kutoa elimu ya amali unaotambulika pamoja na kuwa na miundombinu ya kutosha kwa biashara na mizuri ikiwemo uwanja wa ndege, bandari na barabara hatua ambayo inaifanya Sharjah kuwa ni kituo muhimu cha biashara.

Nae Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazurui aliihakikishia Jumuya hiyo kuwa Zanzibar ina Sera na mipango madhubuti ya biashara na uwekezaji iliyoweka.

Wakati huo huo, Jumuiya hiyo imetoa nafasi ya ufadhili wa masomo kwa vijana wa Zanzibar katika kujifunza mafunzo ya Amali katika Chuo cha Ufundi Sharja.

Akiendelea na ziara yake Sharjah Dk. Shein alitembelea Chuo Kikuu cha Amerika cha Sharja na kupata maelezo ya uendeshaji wa Chuo Kikuu hicho na mafanikio yaliopatikana kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho Dk. Peter Heath.

Katika ziara yake Chuoni hapo, Dk. Shein aliutaka uongozi wa chuo hicho kuja Zanzibar kuangalia maeneo ya kushirikiana kati ya Chuo Kikuu hicho na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Pia, Dk. Shein alitembelea jumba la makumbusho la Dk. Sultan Al-Qasimi na kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu Ali Almarri, Chuo Kikuu cha Sharja cha Tiba na Sayansi ya Afya pamoja na kutembelea jumba la sanaa mjini Sharjah.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.