Habari za Punde

BALOZI SEIF ATEMBELEA MAONESHO YA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHURU

Mama Asha Seif Iddi mke Wa Balozi Seif Ali Iddi akipatiwa maelezo juu ya vitabu vinavyotumiwa na wanafunzi wa sekondari wakati alipotembelea banda la wizara ya elimu katika maonesho ya maadhimisho ya kutimia miaka 50 ya uhuru yanayo endelea katika viwanja vya sabasaba


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisoma Gazeti La Ngurumo la mwaka 1964 lililoandika juu ya mkutano wa kwanza wa marehemu Karume aliyekuwa Rais wa Zanzibar alipozungumza juu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Balozi Seif aliliona gazeti hilo wakati alipotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru viwanja vya sabasaba.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Maendeleo makubwa yamepatikana ndani ya Taasisi Tofauti za Umma na Zile Zisizo za Kiserikali katika kipindi cha Miaka 50 tokea Tanzania Bara ijipatie uhuru wake tarehe 9 Disemba mwaka 1961.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Vyombo mbali mbali vya Habari baada ya kutembelea Mabanda ya Maonyesho ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwenye viwanja vya saba saba Temeke Mjini Dar es salaam.


Alisema Mtiririko mzuri uliowekwa unaonyesha wazi kuwa yapo mabadiliko Kimaendeleo Jambo ambalo hata uchumi wa Taifa umekuwa na kupunguza ukali wa Maisha.

‘‘ Tumepiga hatua kubwa ndani ya kipindi cha miaka 50 na hakuna hata mtu mmoja atakayebisha kwa hilo ’’. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliongeza kusema kwamba mwaka 2014 Zanzibar itasherehekea miaka 50 tokea kufanyika kwa Mapinduzi ya Mwaka 1964. Hivyo Maonyesho hayo ya Uhuru wa Tanzania Bara yanatoa fursa ya kujifunza.

Aliupongeza Uongozi wa Maonyesho ya Biashara Tanzania kwa hatua nzuri ya Maandalizi ya Maonyesho hayo yaliyotoa fursa kubwa kwa Wananchi kuona na kupata kujifunza Taaluma mbali mbali.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Maonyesho ya Biashara Tanzania Bw. Ramadhan Hashim Khalfan amesema Maonyesho hayo yameonyesha sura ya kuvutia kwa vile yamevuka kiwango Bora.

Bw. Ramadhan alimueleza Balozi Seif kwamba vigezo vya Taasisi ya Kimataifa ya Maonyesho vimeeleza Tanzania kuongoza katika kiwango cha Maonyesho Bora ndani ya Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika.

Katika ziara hiyo Balozi Seif alipangiwa kuyatembelea Mabanda ya Maonyesho ya Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Mambao ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Fedha.

Nyengine ni Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
7/12/2011.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.