Habari za Punde

DORIA YAFANYIKA KUDAKA UVUVI HARAMU

Na Othman Maulid

IDARA ya Maendeleo ya Uvuvi Zanzibar, imefanya doria kwa kutumia Ndege, katika Bahari ya Ukanda wa Ghuba ya Minae, kuangalia Uvuvi haramu unaofanyika katika Ukanda huo na Meli za Kigeni za uvuvi ambazo huingia katika bahari ya Zanzibar kwa kufanya shughuli za Uvuvi bila ya Kibali.

Doria hiyo imewashirikisha viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na Katibu wa Ghuba ya Minae, Mohammed Suleiman, ili kujionea jinsi ya doria za baharini zinavyofanyika kwa kutumika ndege, kuangalia uvuvi haramu unavyofanyika kwa kutumia meli za uvuvi za kigeni zinazoingia Zanzibar kufanya shughuli za Uvuvi bila ya Kibali.


Zoezi hilo la doria kwa kutumia usafiri wa ndege, limeongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Doria Idara ya Uvuvi na Maendeleo Kapteni Haji Shomari, limefanyika katika maeneo ya Unguja, Pemba na mwambao wa Tanga, kuona kama kuna chombo kinajishughulisha na uvuvi haramu.

Amesema Idara imeamuwa kuwashirikisha viongozi wa vyombo vya ulinzi ili kupata ushirikiano na uelewa jinsi ya doria za baharini zinavyofanyika, katika ukanda huo wa Ghuba ya Minae.

Amesema doria hizi za kutumia ndege zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kupunguza uvuvi haramu unaofanywa na meli za Uvuvi, katika bahari ya Zanzibar, katika doria hiyo hawakukuta chombo chochote kikijishughulisha na uvuvi katika ukanda huo.

Amewataka wananchi kuondowa wasiwasi wanapoona meli kubwa katika Pwani ya Makunduchi, Paje na Jambiani, na kuripoti kuwa kuna meli za kigeni zinafanya uvuvi katika maeneo hayo, amesema kuna meli hutumia bahari hiyo kwa kusubiri zamu zao kuingia bandarini Dar es Salaam, hutumia eneo hilo kama ni sehemu ya kusubiria.

Amesema doria ya aina hii ina maana sana, pindi wanapoona meli ya kigeni inafanya shughuli za uvuvi,katika maeneo hayo, huchukuwa namba ya meli na kuripoti katika taasisi ya kimataifa inayohusika na mambo ya uvuvi ya IUU, kwa kuchukuliwa hatua za kisheria meli husika.

Amesema Serikali imeandaa maeneo maalum kwa ajili ya kufanya shughuli za uvuvi kwa wananchi wake ili kuthibiti uvuvi haramu unaofanywa na baadhi ya wananchi katika maeneo yao.

Amewataka wafanyabiashara kujitokeza kuwekeza katika maeneo ya Uvuvi, kununu meli za uvuvi kufanya shughuli hii, kwani wavuvi wa Zanzibar hawana uwezo wa kufika katika maji mengi ili kufanya uvuvi wa uhakika, na kupunguza uvuvi unaofanywa katika maeneo hayo kwa hayo.

Ameeleza kwa sasa hakuna meli ya kigeni inayoingia katika maeneo ya Zanzibar kufanya shughuli za uvuvi tangu walipoanza kufanya doria kwa kutumia Ndege, katika bahari kuu na kufanikiwa katika zoezi hilo na Idara yake itazidi kutowa elimu inayotolewa na Mradi wa MACEMP kwa wananchi jinsi ya kupunguza uvuvi haramu na njia mbadala wa uvuvi unaofaa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.