Habari za Punde

MVUA KUBWA ZAIDI KUNYESHA

Tahadhari yatolewa kwa wananchi

Na Mwantanga Ame

HUKU baadhi ya wananchi waliokumbwa na mafuriko wakiendeleza msimamo wa ukaidi kwa kutohama mabondeni, Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA), imebashiri kuwepo mvua zaidi hasa katika kipindi cha mwaka mpya.

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Agnes Kijazi kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa zipo dalili na ishara za mvua kuendelea zaidi na kutahadharisha wananchi kuchukua tahadhari ya kuepuka maafa.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo Mkurugezi huyo, alisema uwezekano kutokea kwa mvua kubwa upo kwa kiasi kikubwa baada ya vipimo vya kuoonyesha ndani ya mwezi huu kuanzia jana kuelekea mwaka mpya kutanyesha mvua hizo.

Alisema hali hiyo inajitokeza kutokana na mwelekeo wa mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa yalioanza kujitokeza katika mwezi huu wa Disemba.

Alisema utabiri unaonesha kuwa katika kipindi hicho unatarajia kuimarika kwenye maeneo mengi nchini na mvua hizo zitaanzia katika ukanda wa Pwani kuanzia leo.

Alisema Mkoa wa Dar es Salaam, mvua hizo zitaweza kunyesha hadi kuingia katika kipindi cha mwaka mpya wa 2012.

Kijazi alisema itatokana na kuanza kujionesha katika mifumo ya hali ya hewa kuimarika kwa hali ya joto katika bahari ya Hindi, sambamba na kuongezeka kwa hewa yenye unyevu nyevu katika misitu ya Congo.

Kijazi, alisema hali hiyo itasababisha kuwapo kwa makutano ya upepo katika eneo la mashariki na Kusini Magharibi mwa nchi kuanzia leo kuelekea mwaka mpya.


Akitaja maeneo ambayo upo uwezekano wa kutokea kwa mvua ni pamoja na Mikoa ya ukanda wa Pwani, ikiwemo Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mtwara, Lindi na kisiwa cha Unguja.

Eneo jengine ambalo alilitaja Mkurugenzi huyo, alisema ni ya nyanda za Juu Kusini Magharibi, ambapo mvua hizo zinatarajiwa kunyesha katika Mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa.

Upande wa Kanda ya kati Mkurugenzi huyo, alisema ni pamoja na mikoa ya Dodoma na Singida na Magharibi mwa nchi, mikoa ambayo inatarajiwa kupata mvua hizo ni ya Kigoma, Tabora na maeneo machache ya nyanda za za Juu Kaskazini Mashariki katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Mara
na Manyara ambayo itakuwa na mvua kubwa.

Kutokana na viwango vilivyoonesha hali hiyo Mkurugenzi huyo alisema, mvua itaongezeka kidogo na inatarajiwa kusababisha kutokea kwa mafuriko na uharibifu wa miundo mbinu.

Kutokana na hali hiyo Mkurugenzi huyo, alindelea kutoa tahadhari ya kuzitaka Mamlaka stahiki katika kusimamia ustawi wa jamii kuendelea kuzingatia utabiri huo na kuweka hadhari itayoweza kuepusha kutokea
kwa athari zitazoweza kutokea wakati mvua hizo zitaponyesha.

Alisema, tahadhari hiyo itapaswa kuzingatiwa utekelezaji wake katika maeneo mengine ya Mji kutokana na mvua hizo zinatarajiwa kunyesha kwa mvua za kawaida.

Hata hivyo, Kijazi alisema Mamlaka hiyo itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya Hali ya Hewa na athari zake na itahakikisha inatoa taarifa na tahadhari kila itapohitajika kufanya hivyo.

Hapo awali Mkurugenzi huyo akitoa tathmini ya mvua iliyonysha wiki iliyopita na kusababisha kutokea kwa mafuriko alisema mvua iliyotokea imevunja rekodi kwani ni ya kiwango kikubwa kilichokuwa hakijafikiwa
tangu mwaka 1954.

Kijazi alisema mvua iliyonyesha kwa kipindi cha siku mbili ilifikia milimita 216 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kwa muda mrefu kwani Wastani wa mvua za kawaida kwa mwezi ni milimita 118.

Kijazi pia alitolea mfano mvua iliyonyesha Desemba 15, 1999 kuwa ilikuwa ni milimita 110.3 na Desemba 16, 2006 ilifikia milimita 108.

Vipimo vya TMA katika mvua zilizonyesha katika Mji wa Dar s Salaam vimeoonesha kiwango cha mvua kilifikia, milimita 156.4 wakati ile ya awali ilikuwa ni milimita 60, huku kituo cha Kibaha mkoani Pwani
kilipima mvua milimita 67.8,” kiwango ambacho kilikusanywa kwa mvua zilizonyesha kuanzia asubuhi hadi saa 3.30.

Mvua hizo hadi sasa zimesababisha vifo vya watu 40 huku wengine wakikosa makaazi na kulazimika kuishi katika makambi maalum na thamani zao kupotea.

Mji wa Unguja hadi saa nane mchana jana umeonekana kuwapo kwa wingu lililotanda kuashiria uwepo wa kunyesha kwa mvua hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.