Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wafuasi wa Chama hicho na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya demokrasia kibandamaiti mjini Zanzibar.
Hassan Hamad (OMKR).
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amezungumzia tena baadhi ya mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kutoa maoni ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwataka viongozi na wananchi kuungana katika kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano.
Amesema iwapo Wazanzibari wataungana na kuwa na sauti moja juu ya jambo hilo, kauli yao itakuwa na nguvu na upande wa pili wa Muungano utalazimika kuheshimu maamuzi hayo ya wazanzibari.
“Viongozi na wananchi wote tushikamane na tuweni na kauli moja juu ya jambo hili, na kamwe tusikubali kugawanywa kwa maslahi ya nchi yetu”, alisema Maalim Seif.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo katika viwanja vya demokrasia Kibandamaiti mjini Zanzibar wakati akiwahutubia maelfu ya wanachama na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliotishwa na CUF.
Amebainisha baadhi ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa na kuingizwa katika katiba mpya kuwa ni haja ya Zanzibar kuwa na benki kuu yake ikiwa ni nia moja wapo ya kudhibiti uchumi wake.
Mambo mengine ni pamoja na Zanzibar kuweza kuwa na sauti huru juu ya sera zake za fedha na uchumi ikizingatiwa kuwa suala la uchumi si katika mambo ya Muungano,sambamba na serikali kuendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka suala la mafuta liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano.
Maalim Seif amefahamisha kuwa Zanzibar inastahiki pia kuwa na uwezo wa kuweka viwango vyake vya kodi, pamoja na kuwa na mitaala yake ya elimu inayoendana na mazingira ya Zanzibar kwa maslahi ya Wazanzibari.
Wiki iliyopita Maalim Seif alielezea umuhimu wa kuwepo utaratibu maalum wa kikatiba utakaoruhusu nafasi ya Urais wa Muungano kutumikiwa kwa awamu kati ya Tanzania bara na Zanzibar, tofauti na utaratibu uliopo sasa ambao hautoi fursa kwa Wazanzibari kuitumikia nafasi hiyo kubwa kabisa ya uongozi nchini.
Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais alitumia fursa hiyo kutoa mkono wa pole kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na baadhi ya wananchi hasa wa mkoa wa Dar es Salaam kupoteza maisha yao, hali iliyosababishwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa.
Amesema mwisho mwa mwezi huu chama chake kimepanga kuzitembelea kambi wanazoishi watu walioathirika na kupoteza makaazi kutokana na mafuriko hayo kwa lengo la kutoa pole na mchango wake kwa waathirika hao.
Wakati huo huo Naibu Katibu mkuu wa CUF Zanzibar Mheshimiwa Ismail Jussa Ladhu amewataka wanachama wa chama hicho kupuuza uvumi juu ya mgogoro ndani ya Chama hicho, na kwamba chama hakina mgogoro na kiko imara wala hakitumbi.
Amesema uvumi huo unaosambazwa kupitia vyombo vya habari umekuwa ukitolewa kwa malengo maalum ya kukivuruga chama, malengo ambayo amesema hayatofanikiwa.
Nae mkurugenzi wa haki za binadamu, habari na mawasiliano ya umma wa chama hicho Bwana Salim Bimani amesema bado serikali ya Muungano haijatoa fursa zinazostahiki kwa Zanzibar katika masuala ya kimataifa ikiwa ni pamoja na kuinyima nafasi za kibalozi nchi za nje.
No comments:
Post a Comment