WAANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kuelekeza nguvu kwenye uandishi wa habari zinazogusa jamii, kuzichambua sera na kuzifanyia utafiti wa kina.
Mwenyekiti mstaafu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (Zanzibar Press Club), Enzi Talib aliyasema hayo alipokua akifunga mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya Zanzibar yaliyofanyika katika kituo Kituo cha Elimu Mbadala Rahaleo.
Alisema endapo waandishi hao wataandika habari zao kwa umakini zinazozingatia uchunguzi zaidi, wataweza kuipa habari jamii ambazo zinagusa matatizo yanayowakabili katika jamii.
Aidha aliwasihi waandishi hao kuwa wakweli wanapotoa taarifa zao ili kuweza kuwatatulia matatizo yao wananchi yanayowakabili katika vijiji vyao.
Hata hivyo aliwasisitiza kutotosheka na elimu waliyokuwa nayo badala yake kujiendeleza zaidi ili waweze kuwa na uwelewa wa kile wanachokiandika na kukitolea taafifa katika chombo chake husika.
“Sisi kama waandishi wa habari basi tuwe na elimu ya kutosha katika kuandika habari zetu ili zimeweze kuwa na uhakika wa kile tunachokiandika kwenye radio zetu ama magazeti yetu kwa lengo la kuhabarisha watu zaidi”, alisema Enzi.
Aidha alisema kuwaelimisha jamii kwa mambo yakinifu yaliyofanyiwa utafiti wa kina ili jamii nayo iweze kuelimika kwa kupokea habari zilizokuwa za kweli zisizokuwa na shaka.
Alifahamisha kuwa tasnia ya habari hivi sasa inakabiliwa na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano, yanavyokuwa katika dunia hivyo aliwaasa wanahabari hao wabadilike kwa kuendana na mabadiliko hayo ili waweze kuandika habari zao kwa uhakika.
Nao washiriki wa mafunzo hayo waliahidi kuyafanyia kazi mafunzo waliyopatiwa kwa kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata kwani wameweza kujua na kupata uwelewa wa kutosha katika mafunzo hayo.
Mafunzo hayo ya siku nne kwa waandishi wa habari yenye lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa Zanzibar kwa kuweza kujua sera, uchambuzi na bajeti yameandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari wa Zanzibar (ZPC) na kusimamiwa na UTPC.
No comments:
Post a Comment