Habari za Punde

Mlioacha Dawa za Kulevya Shawishini Wenzenu – Mama Asha

Na Mwantanga Ame

MKE wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Seif Iddi, amewataka vijana walioamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya, kutumia nafasi yao kuwashawishi vijana wenzao ambao bado wanatumia dawa hizo kujiunga na vituo hivyo ili waondokane na vitendo hivyo.

Mama Asha, aliyasema hayo alipowakabidhi vifaa mbali mbali vya ufundi na vyakula vijana wanaoishi katika nyumba ya ‘Detroit Soba House’ ya Mpendae Wilaya ya Mjini Unguja.

Mama Asha, alisema hatua waliyoichukua kuamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ni jambo la kishujaa, lakini bado wanahitaji kuona wanatumia nafasi yao kutoa ushawishi kwa vijana wengine ambao bado wanaendelea kutumia dawa hizo kuachana na vitendo hivyo.

Alisema nia ya serikali kuona inatumia nguvu kazi ya vijana hao katika kulijenga taifa lao na haitapendeza kuona kuna kundi la vijana ambao bado nguvu kazi yao inapotea kwa kutumia dawa za kulevya.

Alisema kitendo cha vijana walioamua kuchana na dawa hizo ni mwanzo mzuri wa serikali kupunguza tatizo la dawa hizo hapa nchini kutokana na hivi sasa kuamua kupambana na dawa hizo.

Alisema ili mapambano hayo yaweze kuwa na mafanikio yanahitaji nguvu za pamoja na haitakuwa busara kuliacha kundi jengine likiwa linaendelea kutumia dawa hizo kwani linaweza likasababisha kutomalizika ama kuwaambukiza vijana wengine kuingia katika vitendo hivyo.

Aidha, Mama Asha, aliwataka vijana hao kukataa kuitwa jina la ‘MATEJA’ kwani linawashushia hadhi na lenye kuwatia kasoro mbele ya jamii kwani wao ni sawa na binadamu wengine na hawana haki ya kukubali kuitwa majina yanayoweza kuwabagua.

Hata hivyo, Mama Asha, aliwataka wazazi ambao watoto wao wanaotumia dawa za kulevya kuona wanawapa msaada baada ya kuwaacha kuendelea na vitendo hivyo.

Mama Asha, aliwapongeza vijana hao na kuwataka kuendelea kujifunza mambo ambayo yataweza kuwasaidia kuwa raia wema na wenye ujuzi wa kujituma wenyewe baada ya kutoka katika nyumba hizo.

Kutokana na jitihada zao hizo Mama Asha alisema atakuwa tayari kuwaunga mkono kwa kuwapatia misaada mbali mbali ikiwa pamoja na kuwapatia Mwalimu ambaye atawapa mafunzo ya ujasiria Mali.

Mapema kijana Ahmeid Issa, akisoma risala yao alisema bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo serikali inahitaji kuona inawasaidia hasa watoto wa kike ambao wanaishi ndani ya nyumba hizo.

Alisema tatizo kubwa ambalo watoto hao wa kike ingawa wameamua kuachana na dawa hizo, lakini hujikuta wanarudia vitendo hivyo kutokana na hali ya maisha inayowakabili kwa vile tayari wanafamilia zinazowategemea kutokana na kuwa na watoto wadogo.

Alisema vijana hao huamua kurudia kuuza miili yao ili waweze kupata mahitaji muhimu ya kujikimu, jambo ambalo huwaingiza tena katika utumiaji wa dawa za kulevya kwa vile huwa hawana kitulio ndani ya nyumba hizo wakati wakiwa wanapewa tiba.

Ili kuwasaidia vijana hao alisema ni vyema serikali ikafikiria kuwasaidia kwa kuwapatia msaada wa ulezi wa watoto wao katika nyumba za kulelea watoto katika kipindi maalum hadi wazazi wao waweze kuwa vizuri kimaisha kuishi na familia zao.

Alisema katika vituo vya SOBA House hivi sasa kuna vijana 1,162 kwa Unguja na Pemba ambapo kati ya hao 43 ni wanawake na walio safi baada ya kutoka kwenye vituo hivyo ni asilimia 47.

Hata hivyo kiongozi huyo, alisema wanakabiliwa na tatizo kubwa la baadhi ya wazazi kuwakataa watoto wao baada ya kutoka ndani ya nyumba hizo huku wengine wakishindwa kulipia gharama za matunzo na kuwapo kwa tatizo la lishe duni kwa watoto waliozaliwa na wanawake wanaotumia dawa za kulevya jambo ambalo huwasababishia kupoteza maisha.

Akitoa shukrani zake Mlezi wa vituo hivyo, Fatma Sukwa, alisema bado vijana wanaoishi katika nyumba hizo wanahitaji kupatiwa msaada zaidi ili waweze kuendelea kimaisha na kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.