Ni baada ya kumtaja ‘mchawi’ anayemzuia Maximo
Apewa siku saba kuthibitisha tuhuma hizo au…
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIBU wa Baraza la Wazee wa klabu ya Yanga Ibrahim
Akilimali, ameingia matatani kufuatia shutuma alizotoa dhidi ya mwana blogu
Shafii Dauda, kwamba ndiye anayetia fitina ili Marcio Maximo asije nchini
kuifundisha timu hiyo.
Akilimali aliitisha mkutano na waandishi wa habari
Jumatatu Juni 18 mchana kwenye makao makuu ya Yanga mtaa wa Jangwani jijini Dar
es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, alimshutumu Dauda kwamba amekuwa
akiwasiliana na Maximo na kuichongea klabu hiyo.
Kupitia mkutano huo, mzee Akilimali alinukuliwa akisema
kwamba yeye (Shaffii Dauda), ndiye kikwazo cha ujio wa kocha wa kimataifa wa
Brazil, Marcio Maximo ambaye Yanga
inataka kumleta nchini.
Akilimali aliweka wazi kuwa Dauda amekuwa akiwasiliana
na Maximo, na kumwambia mambo mengi ya uongo kuhusu Yanga ili aweze kutimiza
lengo lake la kumuona kocha huyo hatii mguu klabuni humo.
Aidha amenukuliwa akisema kwamba Dauda amekuwa akimtumia ujumbe mfupi wa simu,
barua pepe na kumpigia simu Marcio Maximo kumwambia asiende Yanga kwa kuwa timu
hiyo ni maskini na ina madeni.
Katika maelezo yake, Akilimali pia amesema, Maximo amewatumia ujumbe viongozi wa Yanga
akiwaambia kuwa, Dauda anamsumbua sana juu ya suala hilo hivyo sasa anaogopa
hata kupokea simu kutoka Tanzania
kutokana na usumbufu wa mwandishi huyo.
Akizungumzia kadhia hiyo, Dauda amesema, akiwa na akili
timamu na kukiwa na uhakika kuwa hakulazimishwa na mtu, mzee Akilimali alimtupia
shutuma nzito ambazo anadiriki kuziita za uongo ambazo zinaweza au
zimeshafanikiwa kuharibu jina lake kama mwandishi wa habari pia binadamu wa
kawaida.
Dauda amefahamisha kuwa, kauli za Katibu huyo zimelenga kumharibia sifa yake
nzuri aliyojijengea kwa kutumia nguvu na kufanya vizuri kazi yake.
Amesema kuwa, kamwe hawezi kuzinyamazia tuhuma hizo nzito
na chafu dhidi yake, na kuziacha zipite hivi hivi, na ndio maana ameona vyema
azilitolee majibu.
Amedai kuwa tuhuma hizo sio tu zinaweza kumchafua, bali
pia zinamgombanisha na mamilioni ya wapenzi na wanachama ya klabu ya Yanga
pamoja na wapenzi wote wenye kupenda maendeleo ya mchezo wa soka hapa nchini.
Amesema yeye na wanamichezo wengine, wamekuwa mstari wa
mbele kupigania maendeleo ya michezo hapa nchini hususan soka, hivyo kwao, ujio
wa Maximo wanauona ungeweza kuisaidia klabu hiyo pamoja na nchi kwa ujumla.
Amempa mzee huyo siku saba kuthibitisha madai hayo kwa ushahidi wa vielelezo ambavyo
amedai anavyo, na iwapo atashindwa, itabidi aitishe tena mkutano wa waandishi
wa habari kama alivyofanya awali, ili akanushe aliyoyasema na kumuomba radhi la
sivyo sheria itachukua mkondo wake.
Ah.. huyu mzee naye, keshakua mtata sasa! haya ndio matatizo ya kuishi bila ya shughuli inayotambulika.
ReplyDeleteFitna ndizo zinamueka mjini!