Na Ameir Khalid
TIMU ya Mkoa wa Mjini Magharibi, imeendeleza ubabe kwenye mashindano ya Copa Coca Cola, baada ya jana kuichapa Iringa magoli 3-0, katika mchezo uliopigwa uwanja wa Nyumbu Kibaha wakati wa asubuhi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Zanzíbar (ZFA) Wilaya ya Mjini Yahya Juma Ali, akizungumza na Zanzíbar Leo kwa njia ya simu mara baada ya pambano hilo, aliwataja wafungaji wa magoli hayo kuwa ni Salum Songoro ‘Kalou’ aliyezifumania nyavu katika dakika ya 21.
Wengine ni Abdallah Salum ‘Sebo’ aliyepachika bao la pili mnamo dakika ya 27, huku kitabu cha magoli kwa watoto hao wa RC Abdallah Mwinyi, kikifungwa na Kitwana Hassan aliyeandika goli la tatu katika dakika ya 70.
Kwa matokeo hayo, timu ya Mkoa wa Mjini Magharibi, imefikisha pointi sita, magoli saba ya kufunga huku nyavu zake zikiwa hazijahujumiwa.
Miamba hiyo iliyowahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka juzi, leo inatarajiwa kushuka tena dimbani kuivaa timu ya Mkoa wa Shinyanga, katika uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
Wakati Mjini wakiendeleza dozi, ndugu zao Mkoa wa Kusini Unguja, wameendelea kutoa takrima baada ya kukubali kipigo cha magoli 2- 1 mikononi mwa Shinyanga, mchezo uliochezwa uwanja wa Tamko, Pwani.
Nayo timu ya Mkoa wa Kaskazini Pemba ikatoshana nguvu kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Manyara.
No comments:
Post a Comment