Habari za Punde

Mwakilishi ahoji udhamini wa TBL

Na Mwantanga Ame
HATUA ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kuingia mkataba wa udhamini wa ligi na kampuni ya TBL kupitia kinywaji chake cha Grand Malt, imezua mjadala katika Baraza la Wawakilishi.

Aliyeibua hoja hiyo, ni Mwakilishi wa jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayoub, ambaye alitaka kujua sababu za serikali kukubali udhamini huo, huku ikifahamu vyema kwamba msingi wake umetokana na kampuni inayotengeneza pombe.

Hata hivyo, akijibu suali hilo, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo kabla kuhamishiwa kwengine Abdilahi Jihad Hassan, alisema udhamini huo wa TBL haujavunja amri ya serikali inayokataza michezo kudhamiwa na kampuni za pombe.

Alisema udhamini huo hauhusiki na pombe bali umetimia kinywaji baridi ca Grand Malt ambacho pia kinazalishwa na kampuni hiyo.

Jihad amekiri kuwa kaampuni ya TBL inazalisha pombe lakini akasema pia huzalisha vinywaji vitatu kikiwemo Grant Malt ambacho hakina kilevi na ndicho kitakachodhamini ligi kuu ya Zanzibar kwa misimu mitatu ijayo.

Aidha alisema, hiyo si mara ya kwanza kwa kampuni ya TBL kudhamini michezo hapa Zanzibar kwa kutumia kinywaji hicho, kwani ilishawahi kufanya hivyo kwa timu ya Baraza la Wawakilishi ambayo Mjumbe aliyeuliza suala hilo ndiye mlinda mlango wake.

Mapema, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Bihindi Hamad Khamis, akijibu suali la msingi la Mwakilishi huyo, alisema fedha zinazotolewa kwa udhamini wa ligi hiyo, zitaweza kuwanufaisha wachezaji pamoja na klabu zinazoshiriki ligi kuu ya Zanzibar kuanzia msimu wa mwaka huu unaotarajiwa kuanza mwezi wa Agosti.

Bihindi pia, alisema ni jukumu la Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa katika mkataba huo, yanatekelezwa ipasavyo ili kuwasaidia wachezaji wa Zanzibar.

Alieleza kuwa, bado serikali itaendelea kusimamia marufuku iliyoweka kwa udhamini wa kampuni za pombe ili kuwaepusha vijana na athari zinazoweza kupatikana kutokana na ulevi hasa kwa kutangaza biashara za pombe michezoni.

“Kinachokatazwa sio jina la kampuni bali ni matangazo ya ulevi, lakini udhamini huo ni wa kinywaji baridi cha Grant Malt ambacho hakileweshi, hatua hiyo isilinganishwe na dhana ya kukataa kula nyama ya nguruwe huku mchuzi wake ukinywewa”, alisema Naibu huyo.



2 comments:

  1. Tusijaribu kuhalalisha haramu kwa ajili ya maslahi.Tunafahamu wazi kuwa kinywaji hicho kinatengenezwa na kampuni ya ulevi na kutangaza bidhaa zake ni kushiriki katika kuendeleza uharamu.
    Suala la msingi iwapo mtu anauza pombe kama ni ajira kwake na hainywi anakuwaje katika hukmu ya uhalali wa mapato?

    ReplyDelete
  2. Hawa wawakilishi wengine..wanapata hizo rizki zao tu!
    Badala ya kuzungumzia shida za maisha zinazowakabili wanachi ikiwa ni pamoja na ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo wanatuletea pumba?

    Visiwa sasa hivi vinakabiliwa na matatizo lukuki kama vile elimu, ardhi, ajira, rushwa, matumizi makubwa ya serikali.

    Kama muakilishi analalamikia udhamini wa MALTA GUINESS ambayo haina hata kilevi basi naahoji pia kudi mbali mbali zinazo lipwa na mahoteli mbalimbali ya kitalii na mabaa ya mitaani, au tuseme akina MBAWALA, KIMTI, RAJU, MERCURY, na wengine wahalipi kodi?

    "Afa..tu..u minunna bibaadhwil kitabi..watkfuruuna..bibaadhwin?"

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.