Na Mwantanga Ame
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi, amesema Serikali inaishughulikia ripoti ya kamati teule
iliyowasilishwa katika kikao kilichopita cha Baraza la Wawakilishi kabla ya
kuitolea maamuzi.
Balozi Seif alisema Serikali haijadharau na
wala haiwezi kuidharau ripoti hiyo, na kubainisha kuwa mara baada ya kufikishwa
rasmi serikalini imekuwa ikifanyiwa kazi ambapo baada ya muda mfupi maamuzi
yatatolewa na taarifa ya maamuzi hayo zitatolewa.
Makamu wa Pili wa Rais, alieleza hayo jana
katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi liliopo Mbweni nje kidogo ya mji za
Zanzibar, alipokuwa akijibu hoja mbali mbali za wajumbe wa Baraza hilo
waliochangia hotuba ya bajeti ya ofisi yake.
Kauli hiyo ya Balozi Seif imekuja kufuatia
wajumbe kadhaa wa Baraza hilo kuinyooshea kidole serikali kuwa imeidharau
ripoti hiyo kutokana na kutotoa maamuzi dhidi ya washukiwa wa tuhuma mbali
mbali zilizobainishwa.
Alifahamisha kuwa serikali haiwezi kuidharau
ripoti hiyo, ambapo katika kipindi kifupi kijacho taarifa rasmi kwa vyombo vya
habari itatolewa juu ya maamuzi yaliyochukuliwa kuhusiana na ripoti.
“Serikali imepokea ripoti ya kamati Teule na
Rais ameisoma ‘page by page’, lakini itabidi tumpe muda kabla ya kufanya
maamuzi sahihi”, Balozi Seif, aliwaeleza wajumbe hao.
Katika hatua nyengine, Balozi Seif aliwataka
Mawaziri kuacha tabia ya kuwadharau Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pale
wanapofika katika wizara zao kutaka kupatiwa huduma mbali mbali.
Alisema wajumbe wa Baraza hilo ni watu
muhimu sana, hivyo si vyema waziri kuwadhararu bali wawape heshima inayostahiki
kulingana na hadhi zao.
Alisema inasikitisha kutokana na kuwepo
taarifa kuwa baadhi ya mawaziri wamekuwa wagumu kuonekana na wananchi na
Wawakilishi, jambo ambalo wanajisahau kama wapo kwa ajili ya kuwatumikia
wananchi.
“Leo unaambiwa kumuona Rais ama Makamu wa
Rais ni rahisi kuliko hata kumuona waziri au Katibu Mkuu, acheni hayo, mpo kwa
ajili ya kuwatumikia wananchi”, alisema Balozi Seif.
Akizungumzia migogoro ya ardhi, Balozi Seif
alisema hajapunguza kasi katika kuishughulikia migogo hiyo, lakini serikali
imewapa nafasi viongozi wa chini ambao ndio wanaonekana kuwa chanzo kuitafutia
ufumbuzi kabla ya kufikishwa kwenye ngazi za juu.
Alisema migogoro ya ardhi ni mingi na ya
muda mrefu, hivyo ufumbuzi wa kuimaliza migogori hiyo unahitaji muda na kueleza
kuwa katika baadhi ya sehemu kazi hiyo imekuwa ikiendelea vizuri.
Aidha Balozi Seif aliwaonya baadhi ya watu
ambao hupita nyumba kwa nyumba na kuchukua orodha ya watu wanaoutaka ama
kuukataa Muungano.
Alisema wananchi waachiliwe watumie nafasi
ya kuchagua wakipendacho katika mchakato wa kutoa maoni ya katiba mpya na
wapewe uhuru kwani kila mmoja ana maoni yake na anapaswa kuhesahimiwa.
Awali waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alisema serikali haina nia ya kumdhulumu
mwananchi katika kumpa msaada katika ajali ya Mv. Spice Islander.
Akizungumzia juu suala la Muungano, alisema
serikali inakiri kuwa hakuna Muungano usiokuwa na matatizo, lakini
kinachohitajika ni kuyafanyia kazi maeneo yenye matatizo na kutatuliwa kwa njia
ya mazungumzo.
Akizungumzia juu ya hali ya siasa, alisema
hali hiyo iko vizuri hasa baada ya Jumuiya ya UAMSHO kukubali kutii sheria za
nchi na ni vyema kwa wananchi kuona wanasameheana kwa yaliotokea ili kuifanya
Zanzibar kupiga hatua za kimaendeleo.
Alisema, sio kweli kama serikali ina mtazamo
wa kuibana Jumuiya hiyo wasitoe maoni yao juu ya katiba mpya kwani serikali
haina nia hiyo ila inasimamia sheria za nchi.
Wajumbe hao waliipitisha bajeti hiyo kwa
kuidhinishia jumla ya shilingi 22,366,010,000, lakini hata hivyo baadhi ya
wawakilishi walilazimika kusimama wakati wa kupitishwa kwa mafungu ya matumizi
kutaka ufafanuzi zaidi wa hoja zao.
No comments:
Post a Comment