Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 03/07/2012
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Zanzibar Abdillah
Jihad Hassan amesema Serikali ilipitisha
Sheria ya uvuvi ya mwaka 2010 kwa nia njema na siyo kuwakwaza wavuvi lakini kama kuna haja ya kufanyiwa marekebisho Serikali itakaa
na kufikiria cha kufanya.
Hayo yamesemwa na Waziri huyo wakati
alipokuwa akimuwakilisha Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd katika
mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Wavuvi wa Kojani KOFDO uliofanyika Ukumbi wa
Wizara ya Habari Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Amesema yeye hakuwepo Barazani wakati wa
kupitishwa sheria hiyo ila anaamini Serikali haina nia mbaya ya kuwakomoa
wavuvi badala yake inakusudia kuwaendeleza wavuvi ili waendelee kufanya kazi
zao kwa maslahi yao
na taifa kwa ujumla.
Waziri Jihadi amewaahidi wanajumuiya hiyo
kuwa mawazo ambayo wameyatoa katika mkutano huo atayawasilisha kwa Makamu wa
Pili ili kufanyiwa kazi kama ambavyo
wameyatoa.
Awali Mwenyekiti wa Jumuiya ya KOFDO Omar
Mohammed wakati akisoma Risala ya jumuiya hiyo alisema Wavuvi wa Visiwa vya Zanzibar wamekuwa
wakiandamwa na matatizo mengi ambayo yanafanywa na Idara ya Uvuvi ikiwemo
utumiaji wa nguvu za ziada katika kupambana na wavuvi kwa madai ya uvuvi
haramu.
Omar amedai kuwa nguvu hizo hazitumiki
katika kuwaelimisha na kuwawezesha wavuvi kuvua uvuvi halali na kuachana na
uvuvi haramu ambapo pia ameiomba Serikali kuwawezesha wavuvi jinsi ya kuvua
katika bahari kuu.
Ameongezea kuwa kumekuwa na taarifa nyingi
za kutolewa misaada mbali mbali kwa vikundi vya wavuvi wadogo wadogo Zanzibar lakini cha
kusikitisha misaada hiyo haiwafikii wavuvi husika.
Aidha Omari amesisitiza umuhimu wa
kujengewa Soko la kuuzia Samaki jumla na reja reja lenye hadhi sambamba na
Serikali kufikiria kuanzisha Chuo cha Uvuvi Zanzibar .
Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na
Wanajumuiya hiyo ya KOFDO yenye maskani yake Mtoni Unguja ulihudhuriwa pia na wawakilishi
wa wavuvi kutoka mikoa mitatu ya Unguja ambapo pia walielezea matatizo ambayo
wanakumbana nayo katika kazi zao.
IMETOLEWA NA
IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 03/07/2012
No comments:
Post a Comment