6/recent/ticker-posts

Rais Dk Hussein Mwinyi akutana na Waziri wa Hijja na Umrah wa Saudi Arabia


 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi akifanya mazungumzo na Waziri wa Hijja na Umrah wa Saudi Arabia, Mhe. Tawfiq bin Fawzan Al-Rabiah, aliyefika kuonana naye akiambatana na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Mhe. Yahya bin Ahmed Okeish leo tarehe 19 Januari 2026, Ikulu Zanzibar,

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein
Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa kuendelea kudumisha
na kuimarisha ushirikiano wa kindugu na wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili,
akibainisha kuwa ushirikiano huo umejengwa juu ya misingi ya kuheshimiana,
mshikamano na maslahi ya pamoja.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 19 Januari 2026, Ikulu Zanzibar,
alipokutana na Waziri wa Hijja na Umrah wa Saudi Arabia, Mhe. Tawfiq bin
Fawzan Al-Rabiah, aliyefika kuonana naye akiambatana na Balozi wa Saudi
Arabia nchini Tanzania, Mhe. Yahya bin Ahmed Okeish.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameomba Serikali ya Saudi
Arabia kuendelea kuunga mkono Mfuko wa Hijja wa Zanzibar (Zanzibar Hajj
Fund) ili kuimarisha maandalizi na mazingira ya mahujaji wa Zanzibar, pamoja
na kuendeleza ushirikiano katika elimu ya Kiislamu kwa kuongeza fursa za
masomo kwa wanafunzi wa Zanzibar nchini Saudi Arabia. 
Aidha, ameishauri Saudi Arabia kuangalia uwezekano wa kuongeza safari za
ndege kati ya Saudi Arabia na Zanzibar, hususan kipindi cha Hijja.

Kwa upande wake, Mhe. Al-Rabiah ameipongeza Zanzibar kwa mageuzi ya
miundombinu, ikiwemo viwanja vya ndege na barabara, akibainisha kuwa hatua
hiyo imechochea ongezeko la watalii na ukuaji wa uchumi, na ameihakikishia
Zanzibar kuendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments