Habari za Punde

Tume ya Kukusanya Maoni Yasitisha Mikutano


Na Mwandishi Wetu, Da es Salaam

Kufuatia ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokea jana, Jumatano, Julai 18, 2012 katika eneo la Chumbe, Zanzibar, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesitisha Mikutano ya Kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba Mpya iliyokua inaendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam na Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo (Alhamisi, Julai 19, 2012) mikutano iliyositishwa ni ile iliyopangwa kufanyika kuanzia leo (Alhamisi, Julai 19, 2012) hadi keshokutwa (Jumamosi, Julai 21, 2012) katika maeneo ya Wawi, Vitongoji, Chanjamjawiri, Pujini, Gombani na Wara.
“Tume imepokea kwa masikitiko makubwa Taarifa ya ajali ya Meli ya MV SKAGIT na imesitisha Mikutano ya kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba Mpya iliyokuwa inaendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema zoezi la kukusanya Maoni litaendelea kuanzia Jumapili tarehe 22, Julai, 2012 na kuwa ratiba ya Mikutano katika maeneo yaliyositishwa itatolewa baadaye.

Hata hivyo, Tume ya Mabadilikio ya Katiba imesema katika taarifa yake kuwa mabadiliko haya hayahusu mikutano ya kukusanya maoni inayoendelea kufanyika katika mikoa sita (6) ya Tanzania Bara ambayo ni Pwani, Tanga, Dodoma, Shinyanga, Kagera na Manyara. 
“Tume inawaomba wananchi wa Mikoa hii kuendelea kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao,” imesema Tume katika taarifa hiyo na kuongeza:
 
“Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatoa pole kwa wafiwa, majeruhi na wote walioguswa na ajali hii na tunamuomba Mwenye Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi na majeruhi wote wapone kwa haraka,” imesema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.