Na Hafsa Golo
WANANCHI wa Kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja, wameiomba serikali kutowafumbia macho viongozi wa siasa wanaochukua uamuzi ambao umekuwa ukileta athari kubwa kwa wananchi na hauna mustakabali mwema kwa wananchi.
Wakizungumza na gazeti hili, kwa sharti la kutotajwa majina yao huko Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja, walisema uamuzi uliofanywa na kiongozi wao wa jimbo la Mkwajuni wa kuamua kujenga uzio ndani ya nasari ya kuotesha mechi katika Wilaya hiyo, umekiuka utaratibu kwani wakulima wengi wa Wilaya hiyo,wanategemea mbegu kutoka katika kituo hicho na maisha yao kwa ujumla.
Aidha wakulima hao walisema kuwa kitendo alichofanya kiongozi huyo ni miongoni mwa mambo ambayo yanawarejesha nyuma wananchi na kuonesha kutowajali, kwani wakaazi wa eneo hilo tegemeo lao kubwa katika kuendesha maisha yao ya kila siku ni kilimo.
"Hakuonesha kutujali wakulima hana sababu ya msingi kuvuruga eneo la nasari ya mbegu na miti mengine kuikata kwani kama ilikuwa anataka kutia uzio Hospitali mbona nafasi ipo bila ya kuathiri nasari, lakini katumia nguvu zake ili atukomoe sisi wakulima," alisema mmoja ya wakulima.
Naye ofisa mmoja kutoka Wilaya hiyo, ambae hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa anashangazwa na maamuzi yaliofanywa na kiongozi huyo kwani hayakuzingatia umuhimu wa wa kilimo, hivyo aliamua kukata michungwa na michenza ambayo ilikuwa imezungushwa katika eneo hilo kwa ajili ya mbegu.
Pia alisema ameonesha wazi kuwa nasari hiyo haina maana jambo ambalo si sahihi kwani wakulima mbali mbali hufika katika nasari hiyo kwa mahitaji ya miche zilizoatikwa hapo.
"Kila mmoja anafahamu kuwa kilimo kinamkomboa mkulima, mchungwa mmoja unakodishwa kwa shilingi 60,000 na Muembe 150,000, lakini kiongozi huyo yeye anaona hauna faida kwa kuwa labda hajaona kuainishwa katika mapato ya serikali mche mmoja shilingi mia tatu anauziwa mkulima na hii ni kuwasaidia wakulima"alisema
Aidha alishangazwa na kitendo kilichofanyika kwa kuwa wamepita wanasiasa wengi, na wote waliheshimu uwepo wa nasari hiyo, lakini yeye hakuona umuhimu wa kuendelea kuimarika kwa nasari hiyo na kuamua kuihujumu.
"Nasari hiyo ipo zaidi ya miaka 30 hivi sasa na hilo eneo lililojengwa Hospitali ya Kivunge ni la Wizara ya Kilimo na Maliasili na wameruhusu kujengwa kwa kuzingatia umuhimu wa huduma hiyo, pia kuendeleza maendeleo lakini yeye hakuchukuwa busara isitoshe wamepita wanasiasa mbali mbali na waliheshimu"alisema
Nasari hiyo imeoteshwa mbegu za mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na minazi, mikarafuu, Miembe, Mivinje, Michungwa, Michenza, Mipapai, Mapesheni, Mikeshia, Miburugamu ambapo wakulima kutoka maeneo tofauti ya Mkoa wa Kaskazini Unguja wanafika hapo kwa ajili ya mahitaji ya miche na shamba hilo lenye ukubwa wa hekta nne.
No comments:
Post a Comment