Habari za Punde

Bodi Mafunzo ya amali izalishe ajira

Na Hafsa Golo
WAZIRI wa Elimu Mafunzo na Amali Ali Juma Shamuhuna amewataka wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo majukumu yao ili waweze kujenga misingi imara itakayowezea kuinua vipaji vya mafuzo ya amali na kukuza sekta ya ajira nchini.

Waziri Shamuhuna alisema hayo alipozinduwa bodi ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali katika ukumbi wa wizara hiyo huko Mazizini nje ya Manispaa ya Mji wa Zazibar.

Alisema usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa majukumu utafikia malengo na dhamira ya Elimu Mafunzo ya Amali katika visiwa vya Unguja na Pemba na vijana wengi wataweza kujiajiri wenyewe na kuondokana na kutegemea ajira kutoka serikalini jambo ambalo limesababisha kuwa na wimbi kubwa la vijana kukua vijiweni na kujiingiza katika vikundi viovu.

Aidha wazii huyo aliitaka bodi hiyo kurudisha huduma za dahalia katika vituo vya mafunzo ya amali vilivyopo Mkokotoni katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na Vitongoji katika Mkoa wa Kusini Pemba ili kuwajenga uwezo.

Aidha alisema miongoni mwa majukumu ya bodi hiyo, ni kuhakikisha matumizi ya pesa za serikali zinatumika vizuri katika wizara ya Elimu ili kuepusha hoja nyingi juu ya udhibiti wa fedha hizo ambazo za baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walikuwa na hoja kuhusiana na matumizi ya pesa.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya Vyuo vya Amali, Dk. Idrisa Muslimu Hija alisema kuwa serikali lazima kutekeleza mipango na mikakati iliyopo ili kuinuwa uchumi kupitia Vyuo vya Mafunzo pamoja na kuwa gharama za uendeshaji ni ghali.

“Uendeshaji ni ghali lakini nchi zote zilizoelekeza zimeweza kuinua uchumi kupitia mafunzo ya amali”, alisema mkurugenzi.

Shamuhuna alisema malengo na dhamira hayawezi kufikiwa kama serikali haitoimarisha mazingira madhubuti ikiwemo vifaa walimu wa kutosheleza ambao wenye sifa za kufundisha.

Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Mohammed Hafidh Khalfan alisema malengo yanaweza kufikiwa iwapo mashirikiano ya pamoja kati ya wizara ya Elimu na wajumbe wa bodi hiyo ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hivyo dhamira ya jina la mafunzo ya amali litafikiwa.

Aidha alisema kuwa,imefika wakati kwa serikali kutafute mbinu mbadala ambazo zitawawezesha vijana wanaomaliza mafunzo ya amali kupewa mitaji ili waweza kujiajiri wenyewe na kuitumia elimu waliopewa kwa ufanisi.

“Kama Malaysia baada ya kumaliza masomo vijana wa mafunzo ya amali,serikali iliamua kuwatafutia njia za kupata pesa za kuimarisha kazi zao hivyo wameweza hata kuondosha tatizo la ajira na kuwajenga uzalendo ambao hawapotayari kufanya kazi nje ya taifa lao”, alisema.

Naibu Katibu wa wizara ya Elimu, Abdalla Mzee alisema kuwa wizara hiyo kupitia Mradi wa Elimu Mbadala Amali utawapatia vijana wote mkopo ili waweze kujiajiri wenyewe na kuitumia elimu waliopatiwa kwa vitendo, ,vijana hao wanatarajiwa kumaliza mafunzo yao katika vyuo vya amali mwishoni mwa mwaka huu.

“Tutawapatia wanafunzi mikopo ili waweze kujiajiri wenyewe kwa wale wanaotaka pesa zipo za kutosha kabisa”, alisema.

Naye mjumbe mmoja wa bodi Dk. Salim Said Nasser alisema maslahi madogo kwa wafanyakazi yanasababisha kuzorota kwa ufundishaji kwani wataalamu wengi wenye sifa huamua kwenda nchi jirani kufanya kazi kwa kufata maslahi yalio bora.

Pia alisema hivi sasa nchi ipo katika mashindano ya Afrika Mashariki hivyo ni vema kuwaandaa vijana kielimu na kuwawezesha kuwakilisha taifa wakiwa na sifa ili yafikiwe malengo.

“Bila ya kujipanga na kuwapatia maslahi bora wataalamu tutajenga nyumba ya karata”alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.