Habari za Punde

Maalim Seif ahudhuria na kuifunga Darsa Msikiti Gofu

Na Hassan Hamad, OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewataka waislamu nchini kuendeleza darsa zilizoasisiwa na masheikh mbali mbali, ili kuwaenzi masheikh hao kwakujenga maadili mema kwa jamii.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akifunga rasmi darsa ya Ramadhan katika Masjid Goff uliopo Mkunazini mjini Zanzibar.

Amesema Masheikh waliopita wamefanya kazi kubwa ya kuanzisha na kuendeleza darsa katika misikiti mbali mbali ya Zanzibar, na kutaka darsa hizo ziendelezwe kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Makamu wa Kwanza wa Rais ametumia fursa hiyo kuiombea nchi na wananchi wake amani, na kutoa wito kwa wananchi kuiendeleza amani iliyopo, ili kushajiisha harakati za maendeleo.

Mapema akitoa darsa katika msikiti huo, ustadh Mohd Said Al-Beiz amesema darsa hiyo ilianzishwa zaidi ya miaka mia moja iliyopita, na kwamba imekuwa ikiendelea vizuri tangu kuasisiwa kwake.

Amefahamisha kuwa darsa hiyo hufungwa kila ifikapo mwezi 27 Ramadhan, ili kutoa fursa kwa wanadarsa kujiandaa na sherehe za Sikukuu.

Nao wazee wa Msikiti huo wameiomba serikali kuweka mikakati imara ya kuwadhibiti wageni kuweza kuheshimu utamaduni wa Zanzibar yakiwemo mavazi hasa inapofika kipindi cha Ramadhan.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.