Na Ramadhan Makame
WAZIRI wa Biashara Viwanda na Masoko, Nassor
Ahmed Mazrui amesema utafiti wa kuigeuza Zanzibar kuwa eneo tengefu la kiuchumi
‘Special Economic Zone’ (SEZ), umekamilika na kubainisha maeneo
yatakayoiwezesha kukua kiuwekezaji na kiviwanda.
Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi
wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar alipokuwa
akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo.
Waziri huyo alisema utafiti huo umebaini
kuwa ipo fursa ya Zanzibar kukua kiviwanda ambavyo vitazalisha bidhaa
zitakazosafirishwa nje na kuweza kukuza uchumi wake.
Alifahamisha kuwa utafiti huo umebaianisha
kuwa Zanzibar inayo fursa kuwa eneo muhimu la kusafirisha bidhaa za mazao ya
kilimo, usafirishaji wa bidhaa zilizosarifiwa pamoja na kuwa eneo la
usafirishaji wa bidhaa katika bandari.
Waziri huyo alisema mkakati wa kuifanya
Zanzibar kuwa eneo tengefu la kiuchumi linahitaji kwenda sambamba na uwekaji wa
miundombinu hasa katika bandari na viwanja vya ndege pamoja na kuwepo maeneo
maalum kwa ajili ya uendelezaji mazao ya kilimo.
Akizungumzia kudorora kuimarika kwa sekta ya
viwanda, waziri huyo alisema lipo tatizo la ukosefu wa mitaji kwa wazalishaji
ikiwemo kukosekana kwa benki ya uwekezaji katika sekta ya viwanda.
Aidha sababu nyengine alisema ni pamoja na
ukosefu wa miundombinu hasa ya maji na umeme wa uhakika katika maeno ya Fumba
na Micheweni ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji.
Akielezea tatizo la wafanyabiashara wa
Zanzibar kutozwa kodi mara mbili pale wanapopeleka bidhaa Tanzania bara, waziri
huyo alisema suala hilo lilijadiliwa na kuchukuliwa hatua za kisera lakini bado
tatizo hilo lipo.
Alifahamisha kuwa katika kulishughulia suala
hilo ni vyema wafanyabishara wakawasilisha vielelezo vya kutozwa kodi ili iwe
msingi wa kujenga hoja katika majadiliano ya kero za muungano.
Kuhusu mfumo wa bei alisema mwaka 2011
ulifikia 14.7 ambapo ulichangiwa zaidi na uwepo wa hali ya ushindani mdogo wa
ndani na masoko ya nje kuyumbisha hali ya bei.
Waziri Mazrui alisema kuanzia Februari hadi
mwezi Juni kulishuhudiwa wimbi la usafirishaji wa bidhaa za vyakula muhimu
kutoka Zanzibar kupelekwa Dar es Salaam, ambapo hali hiyo inatokana
wafanyabiashara hao kufuatia bei katika soko.
Hata hivyo alisema suala hilo limedhibitiwa
kwa kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama kuzuia usafirishwaji wa vyakula nje
ya Zanzibar pamoja na kutumia sheria kwa wale waliokamatwa wakisafirisha bidhaa
hizo.
Akiwasilisha maoni ya kamati ya kamati ya
Fedha Bishara na Kilimo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Abdalla Mohammed Ali
alisema jitihada kubwa zinahitajika kuchukuliwa ili Zanzibar iweze kusafirisha
nje bidhaa.
Makamu huyo aliipongeza serikali kwa
kuongeza bei ya karafuu hali iliyofana wakulimwa kuhamasika kuuza karafuu zao
katika shirika la ZSTC.
Aidha kamati hiyo imeiomba serikali
kuliangalia upya bei ya mwani kwani iko chini pamoja na kuishauri wizara hiyo
kuwa makini suala la mfumko wa bei ambao umekuwa ukiathiri wananchi.
Aidha Makamu huyo aliitaka serikali itoa
maelezo juu ya mgogro wa kiwanda cha sukari kilichopo Mahonda kwani kamati tatu
zimeundwa lakini hakuna taarifa zozote.
Akichangia bajeti hiyo Mwakilishi wa jimbo
la Magomeni, Salmin Awadh Salimin alisema sekta ya viwanda ndio roho ya uchumi
wa nchi lakini suala la kuimarisha viwanda limekuwa nyimbo.
“Viwanda vilivyopo havijaweza kuchangia
uchumi, naona bado tunaifanyia mzaha sekta hii, haijaonesha mchango wowote
katika maendeleo ya uchumi”,alisema.
Naye Mwakilishi wa jimbo la Uzini, Mohammed
Raza alimtaka waziri huyo asifumbie macho wala kulfanyia mzaha suala la
kuingizwa vyakula vilivyomaliza muda wake.
Aidha Mwakilishi huyo alisema yupo tayari
kutoa mkopo hata wa shilingi milioni 200 bila ya riba kwa wakulima, wafugaji na
wafanyabishara ili waendeleze shughuli zao.
Naye Asha Bakari Makame alitaka kujua
vikwazo vinavyochangia uwepo urasimu wa kupelekwa mchele kisiwani Pemba, pamoja
na kutaka kujua sababu za kwanini ZSTC haijaundiwa bodi.
Aidha alimtaka waziri wa wizara hiyo kutoa
sababu ya kutokufungwa kwa shirika la Magari ambalo badala ya kuuza linachuuza
kutokana na kushindwa kujiendesha.
Waziri huyo aliomba kuidhinishiwa jumla ya
shilingi milioni 5,580 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ikiwa ni kwa ajili ya kazi
za kawaida na kazi za maendeleo.
No comments:
Post a Comment